Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linamshikilia na Kumhoji Frey Cossey (51) Mkazi wa Dodoma na Mbezi beach kwa kuchapisha vitisho kupitia mitandao ya kijamii, dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima.
Aprili 28, mwaka huu Cossey aliandika ujumbe wa kumuonya Padri Kitima ulisomeka “Mwambieni Kitima iko siku ataingia kwenye 18 hatokaa asahau Tanzania, muacheni ajifanye mwanasiasa. Mfikishieni message siku si nyingi atapata anachokitafuta dawa yake iko jikoni atakuja kuozea jela”.
Hata hivyo Aprili 30, 2025 Padri Kitima alishambuliwa kwenye makazi yake Kurasini lilipo Baraza hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 05, 2025, Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kuwa mtuhumiwa huyo alichapisha ujumbe huo wa kitisho mtandaoni siku chache kabla ya tukio la shambulio, jambo ambalo limeifanya Jeshi la Polisi kumchukulia hatua za haraka.

Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wake kwa kina, likishirikiana na vyombo vingine vya usalama, kuhakikisha waliohusika wote wanapatikana na kuchukuliwa hatua stahiki.
“Mpaka sasa tayari tunawashikilia watu wawili kuhusiana na tukio hili la Padri Kitima na upelelezi wake unaendelea kwa kina, tukishirikiana na vyombo vingine vya usalama, kuhakikisha waliohusika wote wanapatikana na kuchukuliwa hatua stahiki,” amesema Muliro.
Aidha jeshi hilo limewakamata watu watano kwa tuhuma za usafirishaji wa Dawa za kulevya aina ya bangi gunia 60, zilizokuwa zimepakiwa kwenye gari yenye namba ya usajili T 466 EDV aina ya HOWO, lililokuwa na tenki lenye muonekano wa kubeba mafuta yenye usajili T994 EEG.
Watuhumiwa hao ni Nathan Danga maarufu kama Masumbuko, Ali Mussa, Abdala Athuman, Mohamed Chahama na Upendo Mgonja ambapo watafikishwa kwenye vyombo vingine vya sheria haraka iwezekanavyo.
Vilevile Jeshi hilo limemkata David Sanga (39) mfanyakazi wa Bima wa zamani wa Kampuni ya UAP kwa kutoa taarifa za uongo Kituo cha polisi Kigamboni kuwa kuna magari mawili no T 811 DUL Toyota Crown na T 647 DRE Mitsubishi Outlander kuwa magari hayo vifaa vyake mbalimbali vimeibwa.
“Polisi walivyofuatilia walibaini kuwa mtuhumiwa alikuwa amevin’goa na kuvificha nyumbani kwake kwa lengo la kujipatia pesa kwenye makampuni ya bima kwa njia ya udanganyifu.
“Vifaa vilivyon’golewa
na kufichwa ni bampa za mbele na nyuma , window covers ,radio za gari, side mirrors , taa zote za mbele na nyuma , power windows na betri,” amesema
Amebainisha kuwa hatua za kisheria za haraka dhidi ya muhusika zinakamilishwa ili afikishwe kwenye
vyombo vingine vya sheria.
“Jeshi linakemea vikali tabia kama hizi za kutoa
taarifa za uongo kwa makusudi kwa maafisa wa Serikali na halitasita kuchukua hatua za kisheria inapobainika ni kinyume chake,” amesema.