Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara

JESHI la Polisi mkoani Mtwara linamshikilia mkazi wa kijiji cha Lupaso kitongoji cha kadudu Wilaya ya Masasi mkoani humo Victor Fransis (39) kwa tuhuma za mauaji ya mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblise of God (TAG) lililopo kijijini hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara SACP Issa Suleiman amesema tukio hilo limetokea Juni 27, 2025 majira ya saa 12 jioni katika mtaa wa misheni kwenye kijiji hicho cha Lupaso.

Amemtaja marehemu huyo kuwa ni Thomas Rajab (58) ambapo mtuhumiwa wa tukio wakati wakiwa na baadhi ya ndugu zake alikwenda katika kanisa hilo kwa ajili ya kupata huduma ya kiroho kutokana na changamoto ambayo inasadikika kuwa anayo mtuhumiwa huyo.

‘’Mtuhumiwa alikwenda kanisani kwa ajili ya kupata huduma ya kiroho ‘kuombewa’ kutokana na changamoto ambayo inasadikika kuwa anayo mtuhumiwa baada ya kufanyiwa maombi kwa muda mrefu mtuhumiwa alionesha kuchoka’’amesema Suleiman

Ameongeza kuwa,  ‘’Ndugu wa mtuhumiwa kwa kushirikiana na marehemu waliamua kumrejesha nyumbani kwa ajili ya kuendelea na maombi walipokaribia nyumbani kwa mtuhumiwa, mtuhumiwa aliruka kwenye pikipiki na kukimbia kuingia ndani na kutoka na panga’’

Aidha baada ya kutoka na panga hilo alianza kumkimbiza marehemu kisha kumkata na panga sehemu mbalimbaliza mwili wake na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo chake.

Mtuhumiwa huyo ni muumini wa kanisa hilo na amekuwa akipata huduma ya kiroho kwa zaidi ya mwaka ikiwa ni pamoja na kuombewa kwa muda mrefu kutoka kwa mchungaji wa kanisa kwa kile kilichodaiwa kuwa na matatizo ya ugonjwa wa kuanguka (Kifafa).