Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anitha Waitara, ametangaza nia ya kuwania ubunge wa Jimbo la Kivule katika Uchaguzi Mkuu ujao, akiahidi kushughulikia changamoto ya miundombinu ya barabara ambayo kwa muda mrefu imekuwa kilio kikubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Waitara, ambaye ni mkazi wa Kivule, amesema uamuzi wake wa kuingia katika kinyang’anyiro hicho umetokana na uzoefu wa moja kwa moja wa kero zinazowakumba wananchi wa jimbo hilo, hususan barabara mbovu na kukosekana kwa madaraja imara wakati wa mvua.

“Jimbo letu la Kivule lililojitenga kutoka Ukonga limekuwa kama limesahaulika. Kwa mfano, kutoka Banana hadi Kivule unaweza kutumia hadi masaa sita, hasa wakati wa mvua ambapo madaraja hukatika kabisa,” amesema Waitara.
Ameongeza kuwa endapo atapewa dhamana ya kuliongoza jimbo hilo kama Mbunge, suala la kwanza kulivalia njuga ni uboreshaji wa miundombinu ya barabara ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi na haraka.
“Nina ari, nina uwezo, na nina uelewa wa kutosha juu ya changamoto za wananchi wa Kivule. Mimi ni mama, mpambanaji ambaye nimekuwa nikijitoa kwa makundi maalum, vikundi vya vijana na taasisi mbalimbali ndani ya Kata za Kitunda, Kivule hadi Msongola,” amesema.
Anitha Waitara anajiunga na orodha ya makada wa CCM waliotangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, huku akitumia uzoefu wake katika jamii kama msingi wa ajenda yake ya maendeleo kwa wananchi wa Kivule.
