Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dodoma

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wiki iliyopita, yaani Februari 12 na 13, 2026 imeandaa mkutano wa mwaka wa vyombo vya habari vya utangazaji jijini Dodoma. Mkutano huu ulikuwa na mjadala mrefu na wa kina, ila niliguswa zaidi na ‘Uchumi wa Vyombo vya Habari.’

Kwanza, nimewashukuru TCRA si kwa mkutano huu tu, bali kwa kuleta mrejesho wa maazimio ya mkutano wa mwaka jana, ambao washiriki walilalamikia ukubwa wa bei za leseni  na mambo mengine. TCRA imejibu kwa kupunguza bei za leseni hizi.

Sitanii, ada za leseni mtandaoni zimepunguzwa kwa kiasi kikubwa. Leseni ya watengenezaji wa maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka Sh 500,000 hadi Sh 50,000. Ada ya maombi (application fee) imepunguzwa hadi Sh 10,000 kwa waombaji wapya.

Kwa wakusanyaji wa maudhui mtandaoni, ada imepunguzwa kutoka Sh 1,000,000 hadi Sh 100,000. Pia serikali imeanzisha aina mpya ya leseni ya “Amateur” kwa ajili ya wanahabari chipukizi waweze kujiandikisha bila  kulipa chochote na kujiendesha kwa mwaka mzima mtandaoni bure.

Vyombo vya habari vikongwe, kwa maana ya redio na televisheni, nao wameambiwa leseni zitapunguzwa tena kama ilivyofanyika mwaka 2022. Kwa hakika TCRA wanastahili pongezi, kwa kuwa wasikivu. Tumezoea maazimio ya mikutano iliyotanguliwa huwa hayapewi hata mrejesho baadhi ya nyakati, ila TCRA wametenda kinyume kabisa na kwa heshima kubwa. Hongereni TCRA.

Sitanii, ukiacha pongezi hizi kwa TCRA, naomba kutoa angalizo kwa taifa letu. Katika safari ya kujenga taifa lenye mshikamano, uwajibikaji na maendeleo endelevu, vyombo vya habari vina nafasi ambayo haiwezi kuchukuliwa na taasisi yoyote nyingine.

Vyombo vya habari ni macho ya wananchi, masikio yao, na daraja pekee linalounganisha serikali na wananchi kwa uaminifu na weledi. Ndiyo maana nasema – tusifanye kosa la kuviacha vife. Tukiruhusu vyombo vya habari kudhoofika au kufa, tutakuwa tumelipa taifa gharama kubwa kuliko tunavyodhani.

Vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya uwajibikaji. Serikali yoyote, hata iwe nzuri kiasi gani, inahitaji mfuatiliaji anayeangalia mwenendo wa matumizi ya fedha, utekelezaji wa sera, na utekelezaji wa miradi. Bila vyombo vya habari huru, rushwa huchanua kimya kimya, mali za umma hupotea bila kelele, na wananchi hukosa taarifa sahihi za kuwafanya washiriki kikamilifu katika uamuzi wa nchi. Vyombo vya habari ndivyo hulinda mlango wa masilahi ya taifa.

Pili, vyombo vya habari ni shule ya umma. Wananchi kupitia magazeti, redio, televisheni na majukwaa ya kidijitali hupata maarifa kuhusu afya, uchumi, kilimo, elimu, sayansi na teknolojia. Bila elimu hii ya kila siku, jamii hushindwa kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia. Taifa lisilo na watu walioelimishwa kupitia taarifa, ni taifa linalokwenda gizani.

Tatu, vyombo vya habari ni muhimu katika kukuza amani na umoja wa kitaifa. Katikati ya uchaguzi, misuguano ya kisiasa au majanga ya kitaifa, habari sahihi huondoa taharuki na kuzuia upotoshaji unaoweza kusababisha migogoro. Vyombo vya habari vinapokufa, nafasi yao hujazwa na uvumi, propaganda na taarifa zisizo na uthibitisho – na hapo ndipo misingi ya amani huanza kutikisika.

Nne, vyombo vya habari ni waajiri muhimu. Maelfu ya Watanzania – waandishi, wahariri, wabunifu wa matangazo, wapiga picha, wahandisi wa sauti na wengine – wanategemea sekta hii kupata kipato. Sekta ikianguka, wengi wanabaki mitaani, na uchumi unapoteza nguvu kazi muhimu.

Sitanii, leo hii vyombo vya habari nchini vinapitia changamoto kubwa. Kupungua kwa matangazo, gharama kubwa za uzalishaji wa maudhui, ugumu wa usambazaji, ushindani kutoka majukwaa ya kidijitali yasiyolipa kodi, na mazingira ya sheria yanayohitaji maboresho, ni changamoto ya kweli. Hatuwezi kuviangalia vikififia kisha tukabaki tunalalamika baada ya kuwa tumepoteza sauti ya jamii.

Suluhisho si kuvizidishia vikwazo bali ni kuviwezesha. Serikali inaweza kuweka mazingira rafiki ya kibiashara, kupunguza kodi zisizo za lazima, kurahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu, na kuwekeza katika mafunzo ya weledi. Vyombo vya habari imara ni msaada kwa serikali iliyopo madarakani na jamii viliyomo.

Sitanii, tunapaswa kuanza utaratibu wa mashirika ya umma kusambaza matangazo kwa uwiano unaozingatia umuhimu wa tasnia, badala ya kuyapeleka sehemu chache. Taasisi binafsi nazo zione umuhimu wa kutangaza kupitia vyombo vya habari vya ndani kama sehemu ya kuimarisha uchumi wa taifa. Taarifa zinazotolewa zinaimarisha mashirika haya. Kama ni wizi unakoma, ila huwa mchango wa vyombo vya habari haukumbukwi.

Vyombo vya habari ni injini ya demokrasia, nguzo ya utawala bora na mhimili wa maendeleo. Tusipovienzi leo, tukivitelekeza ama tukavipunguza nguvu, kesho tutalipa gharama kubwa – kwa kupoteza uwazi, kukosa taarifa sahihi, na kupunguza uwezo wa wananchi kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.

Najua wapo waliojipanga kuvibeza vyombo vya habari, lakini hii ni sawa na msemo wa ‘kitanda usichokilalia hauwezi kujua kunguni wake!’ Wakati umefika tuwe na mjadala wa kitaifa bila kujali vyama vyetu iwapo nchi yetu inavihitaji vyombo vya habari au la! Ni wakati wa kuamka. Tuvilinde, tuviwezeshe, na tuvithamini vyombo vya habari. Taifa lenye habari huru ni taifa lenye nguvu. Rejea Marekani inavyotawala dunia kupitia habari. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827