Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglican Tanzania, Mahimbo Mndolwa ameongoza Ibada ya kumsimika Mkuu wa chuo (Chancellor) wa pili wa Chuo Kikuu cha St John,Askofu Dk Dickson Chilongani.
Askofu Dk Chilongani ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika anachukua nafasi ya Askofu Leonard Mtetemela ambaye amestaafu katika nafasi hiyo aliyoihudumu kwa kipindi cha miaka 18 tangu Septemba 8,2007.

Ibada hiyo imefanyika leo Mei 20,2025 katika Chuo Kikuu cha St John Jijini hapa na kuhudhuriwa na watu mbalimbali ambapo akizungumza katika ibada hiyo,Askofu Mndolwa amemtaka Askofu Chilongani kwa kushirikiana na Kanisa kusimamia suala la mmonyoko wa maadili huku akihoji sera ya maadili ipo wapi.
“Ninyi wenzetu mpo sehemu za kuhoji ndio mtuongoze tunaomba idara ya Theolojia msogee mbele zaidi mmefundisha theolojia sasa tuende kwenye utafunaji wa hoja,hakuna njia ya kulirudisha kanisa isipokuwa kwa njia hiyo ya kupaza sauti,”amesema Askofu Mndolwa
Kwa upande wake Mkuu mpya wa Chuo hicho,Dk Chilongani amesema atapambana kwa kushirikiana na wenzake kuhakikisha chuo hicho kinazidi kupanda kitaaluma Pamoja na suala la mmonyoko wa maadili kwa kuhakikisha wanaozalishwa wanakuwa mfano katika jamii.

“Nimepokea chuo kikiwa katika hali nzuri ya kitaaluma nitahakikisha nashughulikia kwa kina changamoto ya ukosefu wa hosteli ili wanafunzi wakae sehemu nzuri na kuweza kujisomea vizuri,”amesema Askofu Dk Chilongani.


