Shan Dong, China
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewasili nchini China na kutembelea Gridi ya Taifa ya Maji ya China.
Akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Eng Mwajuma Waziri pamoja na watendaji wa sekta Waziri Aweso amefika jimbo la Shan Dong Kaskazini mwa China kuona namna vyanzo vikubwa vya Maji vya mito na Maziwa vimeunganishwa katika gridi ya Taifa ya Maji kutoka Kaskazini mpaka Kusini.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Maji kutekeleza ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji itakayotoa maji kutoka katika vyanzo vikuu vya maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa pamoja na mito ya Rufiji, Ruvuma, Ruvu, Wami, Kiwira, Kagera na Pangani miongoni mwa vyanzo vingine.
Gridi ya Taifa ya Maji ambayo sehemu ya miradi yake ni pamoja na mradi wa maji Tabora, Same-Mwanga-Korogwe, Kiwira na Ziwa Victoria kwenda Dodoma inalenga kuhakikisha uhakika wa maji kwa ajili ya maendeleo ya uchumi.
Mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji ni maelekezo ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ilani ya uchaguzi ikiwa pia ni mwelekeo wa Wizara na Taifa katika kuhakikisha kuwa maji yanachangia katika maendeleo ya Taifa ya uchumi kupitia DIRA 2050.









