Na Mwandishi Wetu

AZAM FC imemtambulisha Florent Ibenge (63) kuwa Kocha Mkuu kwa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza kulingana na mafanikio.

Ibenge, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alikuwa Kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan Kusini, amejiunga Azam akirithi mikoba ya Rachid Taoussi aliyemaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya utambulisho wake, Ibenge alisema amefurahi kujiunga na moja ya timu kubwa Tanzania yenye maono ya kufika mbali na kuahidi kutimiza malengo hayo kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi.

Alisema anatambua ugumu wa ligi ya Tanzania yenye ushindani unaotawaliwa na Yanga na Simba na kueleza akipata ushirikiano mzuri anaona huu utakuwa wakati wa kuwa na kizazi kitakachoimba Azam.

“Malengo ya Azam ni kuwa timu kubwa yenye ushindani na kutwaa mataji, kwa kushirikiana na uongozi, wachezaji pamoja na mashabiki tunaweza timiza ndoto hiyo,” alisema Ibenge.

Aliongeza: “Wapo waliozaliwa wakaikuta Yanga na Simba na kuzifanya timu hizi kuwa na mashabiki wengi, ni wakati sasa wa kutengeneza historia ya kuwa na kizazi kitakachoipenda Azam, si kwa njia nyingine bali kwa kushinda michezo na kushirikiana na mashabiki waliopo”.

Aidha, aliweka wazi kuwa baada ya tathimini atakayofanya wachezaji bora watasalia na wale wasiotosha watapisha ili wengine waje.

Ibenge amewahi kufundisha timu ya taifa ya DRC mwaka 2014 hadi 2019, vilevile AS Vita (DRC) 2012-2021, RS Berkane (Morocco) 2021-2022 pamoja na Al Hilal (Sudan) 2022-2025.

Miongoni mwa mafanikio ni kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN 2016) akiwa kocha wa timu ya taifa wa DRC.

Pia, mwaka 2015 aliifikisha DRC nusu fainali ya Mataifa ya Afrika (AFCON) na kuibuka mshindi wa tatu.

Akiwa na RS Berkane aliibuka bingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika (CAF) mwaka 2022 pia aliiongoza RS Berkane kutwaa Super Cup dhidi ya Wydad Casablanca.

Mwaka 2014 aliifikisha AS Vita fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akimaliza mshindi wa pili.

Hali kadhalika msimu huu aliifikisha Al Hilal hatua ya robo finali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.