Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mbunge mteule wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus (Baba Levo) ametangaza kufanya mkutano mkubwa wa shukrani kwa wananchi wa jimbo hilo wiki ijayo, akisema utakuwa ni tukio la kihistoria litakalolenga kuwashukuru wapiga kura kwa imani waliyoonyesha kwake na kueleza kuwa atautumia mkutano huo kueleza vipaumbele vyake kwa miaka mitano ijayo.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo November 8,2025 Jijini Dodoma amesema mkutano huo utakaofanyika mwishoni mwa wiki utafanyika katika viwanja vya Kigoma Mjini, na utakuwa fursa ya kutoa shukrani rasmi kwa wananchi pamoja na kueleza dira yake ya maendeleo itakayolenga kutatua changamoto za wananchi katika sekta mbalimbali.

“Mkutano huu ni wa wananchi wangu wa Kigoma Mjini,wamechagua na nina deni kwao,nitawashukuru rasmi na kuwaeleza vipaumbele vyangu nitakapoanza kazi ya ubunge,

Nilipojisajili niliombwa nitaje mashahidi watakaoshuhudia nikiapishwa mmoja wapo ni Diamond pamoja na jamaa zangu wa karibu,” amesema Baba Levo.

Aidha, akizungumzia siasa za Bunge lijalo, Baba Levo amesema kura yake ya uspika ipo kwa aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita Azan Zungu kwa sababu ya uadilifu na usawa wake katika utendaji.

Ameongeza kuwa katika nafasi ya Naibu Spika atampigia kura Daniel Sillo, ingawa akishinda mwingine yuko tayari kumuunga mkono kwa maslahi ya Taifa.

Mbunge huyo mteule pia ametoa pole kwa wananchi wote waliopata madhara wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu, akiwataka kuendelea kudumisha amani na umoja ambao ndio msingi wa maendeleo ya Kigoma na Tanzania kwa ujumla.