Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Wakati Jiji la Arusha likikabiliwa na changamoto ya msongamano unaotokana na wingi wa vyombo vya moto kama pikipiki maarufu kama bodaboda, bajaji na guta, bado madereva wa vyombo hivyo wamemuomba Mkuu wa Mkoa huo Kenan Kihongosi kuwaongezea maeneo ya maegesho.

Kihongosi jana amefanya mkutano na madereva hao katika uwanja wa Shekh Amri Abeid ili kujua changamoto wanazokumbana nazo katika shughuli zao za kila siku.

Changamoto kubwa waliyoiwasilisha ni ukosefu wa vituo vya kudumu vya maegesho pamoja na maeneo duni ya kufanyia kazi hali inayowanyima fursa ya kujiendeleza na kuwaweka katika mazingira hatarishi ya kipato na usalama.

Katibu wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Arusha, Hakimu Msemo amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa baadhi ya madereva wa bodaboda hawana leseni za udereva hali inayochangia ajali na kumtaka Mkuu wa Mkoa kutoa tamko kali dhidi ya madereva wanaofanya kazi bila leseni kwani hali hiyo si tu inaleta hatari kwa abiria bali pia inatishia hadhi ya sekta hiyo.

“Hapa Arusha tupo bodaboda zaidi ya elfu 24 lakini changamoto kubwa wengi hawana elimu ya udereva hivyo tunaomba utoe kauli dhidi yao, lakini pia tunaomba wapatiwe mafunzo ya udereva kwani wao ndiyo chanzo kikubwa cha ajali” alisema Msemo.

Kwa upande mwingine Katibu wa Umoja wa Waendesha Bajaji Mkoani humo Salim Lyimo alijikita zaidi kwenye upatikanaji wa maeneo ya kupaki bajaji akisema kuwa maeneo waliyopewa yapo mbali na mji, masoko, hospitali na hoteli za kitalii hivyo kuathiri moja kwa moja idadi ya wateja wao.

“Makadirio ya bajaji zilizopo ni zaidi ya 3,500 huku vituo vikiwa ni changamoto kubwa, hivyo tunaomba tupatiwe maeneo mazuri na tunashauri wenye leseni, makundi maalum pamoja na wenye ulemavu wapatiwe kipaumbele” alisema Lyimo.

Wakati hayo yakiendelea, wadau wa maendeleo ya jiji la Arusha wakiwemo wale wa sekta ya utalii, wanaendelea kusisitiza msimamo wao wa muda mrefu kwamba ongezeko la vyombo vya usafiri kama bodaboda, bajaji, guta na mikokoteni ndicho chanzo kikuu cha msongamano, uchafu na kupotea kwa mvuto wa jiji hilo ambalo ni lango kuu la watalii nchini.

Wakizungumza na Jamhuri hivi karibuni wadau hao waliitaka serikali kufanya maamuzi magumu kuondoa pikipiki na mikokoteni katikati ya jiji pamoja na kupunguza bajaji zilizopo ili ziendane na idadi inayokubalika kisheria.

Walipendekeza kufuata mfano wa Dar es Salaam ambako baadhi ya vyombo hivyo vimepigwa marufuku katikati ya jiji.

Meneja wa LATRA mkoa wa Arusha Omary Ayoub hivi karibuni alithibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kwamba kwa mujibu wa kanuni katikati ya jiji la Arusha zinapaswa kuwepo bajaji 800 tu lakini hadi sasa zipo zaidi ya 3,000.

Alieleza kuwa ongezeko hilo linachangiwa na bajaji zinazotoka mikoa jirani kama Dodoma, Manyara na Kilimanjaro.

Katika kutatua hilo, LATRA tayari imeanza mchakato wa kusajili mabasi makubwa ya abiria na kuacha mabasi madogo aina ya hiace, lengo ni kuhakikisha hadi mwaka 2026, asilimia 80 ya daladala ndogo zitakuwa zimeondolewa katikati ya jiji na kupisha mabasi makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria wengi kwa wakati mmoja.

“Hali hii inachukuliwa kama hatua ya kuboresha usafiri wa umma, kupunguza msongamano na kuiweka Arusha katika ramani ya majiji ya kisasa yanayoheshimu mpangilio wa miji. Na sasa tayari coaster nyingi zimeanza kuchukua nafasi ya hiace kwenye barabara ya Moshi-Arusha, hali inayotoa matumaini mapya kwa wakazi wa jiji hili”

Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Watalii Tanzania (TATO) Wilbard Chambulo, alitumia fursa hiyo kueleza namna miundombinu mibovu, uchafu na msongamano wa magari yanavyowaondoa watalii mjini Arusha mara tu wanapowasili.

Alisema jiji hilo limepoteza mvuto wake na kuwa kama kituo cha kupita kwa haraka kabla ya kuelekea hifadhi za Taifa.

Chambulo alitoa mfano wa Forodhani, Zanzibar akisema eneo hilo limejipambanua kama kivutio kwa watalii kwa sababu ya mpangilio mzuri wa mji, usafi na kutokuwepo kwa msongamano wa magari.

Alisema bila kufanya hivyo Arusha itaendelea kupoteza hadhi yake kama kitovu cha utalii wa Afrika Mashariki.

Aidha alitoa wito wa kuwepo kwa usimamizi mzuri wa mipango miji ili kuhakikisha majengo yanakuwa katika mpangilio, barabara zipanuliwe na maeneo ya ibada, biashara na starehe yatengewe maeneo maalum tofauti na ilivyo sasa ambapo kila kitu kimezagaa bila utaratibu.

Katika hitimisho la kikao hicho, Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa vyombo vyote vya usafiri na wasafirishaji kuhakikisha wanazingatia sheria, wanapata leseni na wanashirikiana na serikali kuifanya Arusha iwe safi, salama na ya kuvutia.

Alisema serikali ipo tayari kuwasikiliza wananchi lakini lazima kila upande uwe tayari kwa mabadiliko ya maendeleo.

“Lazima tutafute njia bora ya kupungumza msongamano, lakini niwaambie ukweli kuhusu ombi lenu la kutafutiwa maegesho katika maeneo mliyoyataja kuwa naenda kulifanyia kazi, nitakaa na wataalamu wangu, kama linawezekana nitawaambia lakini kama haiwezekani nitawaita kama nilivyofanya leo niwamabie ukweli haiwezekani” alisema Kihongosi.