Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ametaja Vipaumbele mahsusi katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali kuwa vitahusisha miradi ya kielelezo, kuimarisha sekta za uzalishaji, huduma za jamii, na kuboresha mazingira ya biashara.

Aidha, Serikali itagharamia maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kutumia fedha za ndani.

Amezungumza hayo Bungeni Leo June 12,2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 na kueleza kuwa bajeti hiyo inalenga kukamilisha miradi ya maendeleo na programu zilizoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Dkt. Nchemba amesema kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuendeleza mafanikio ya Dira ya 2025.

Katika kuongeza mapato, amesema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya risiti za EFD, kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya mamlaka za udhibiti, pamoja na kuimarisha Mfumo wa TAUSI ili kujumuisha vyanzo vyote vya mapato ya Serikali za Mitaa.

Amesema bajeti hiyo itachochea uchumi shindani na shirikishi, kukuza uzalishaji wa viwandani na huduma, kuvutia uwekezaji na biashara, pamoja na kuendeleza rasilimali watu ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Katika hatua nyingine amesema bajeti hiyo itasaidia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya taasisi za umma na mashirika ya Serikali, kuendeleza mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (MKUMBI), pamoja na kuhamasisha matumizi ya njia za kidijitali katika ulipaji wa bidhaa na huduma.