Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imewasilisha bajeti ya mwisho ya kipindi cha kwanza cha uongozi wa Awamu ya Sita kwa mwaka wa fedha 2025/26. Kupitia hotuba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, mafanikio makubwa ya miradi ya kimkakati yamewekwa wazi, ikionesha namna Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyojikita katika maendeleo ya nchi.
Mojawapo ya miradi hiyo ni Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, ambao umekamilika kwa asilimia 99.93 na tayari umeanza kuzalisha umeme.
Amesema Mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati na kuchochea uchumi wa viwanda.
Serikali pia imetangaza kukamilika kwa Daraja la Kigongo–Busisi lenye urefu wa kilomita 3 pamoja na barabara unganishi ya kilomita 1.66 kwa kiwango cha lami.
Daraja hilo linatarajiwa kuzinduliwa tarehe 19 Juni 2025 na litaunganisha vyema mikoa ya Mwanza na Geita.
Katika sekta ya usafiri wa reli,waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imekamilisha kipande cha reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora na kwamba huduma ya usafiri wa abiria imeanza rasmi, ambapo hadi Machi 2025 jumla ya abiria zaidi ya milioni mbili walikuwa wameshasafirishwa, na mapato ya shilingi bilioni 60.25 yakakusanywa.
“Usafiri kwa kutumia SGR umepunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka saa tisa hadi saa tatu. Hali hii imeongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini, ” Amesema na kuongeza;
Ujenzi wa kipande cha tano cha reli ya SGR kutoka Mwanza hadi Isaka (km 341) umefikia asilimia 63.16. Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha mtandao wa reli nchini na kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria, “amesema
Pia ameeleza kuwa Serikali imefanya majaribio ya treni ya mizigo kupitia reli ya SGR tarehe 01 Juni 2025. Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha biashara na kuongeza mapato kwa kutumia njia za kisasa za usafirishaji.
Kwa ujumla, bajeti ya 2025/26 imeweka wazi mafanikio makubwa ya miundombinu, usafiri na nishati ambayo yamefikiwa ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.
