BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limetangaza kuwa Sikukuu ya Eid El-Adh’ha kwa mwaka 2025 itafanyika Jumamosi Juni 7.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 29, 2025 na Katibu Mkuu BAKWATA, Alhaj Nuhu Mruma, kwa Waislamu na wananchi wote nchini, ikibainisha kuwa maandalizi ya sherehe hiyo yanaendelea kufanyika kwa ustadi.

Kwa mwaka huu, BAKWATA imetangaza kuwa sherehe za kitaifa za Eid El-Adh’ha zitafanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Swala ya Eid itaswaliwa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI, uliopo Makao Makuu ya BAKWATA Kinondoni kuanzia saa 1:30 asubuhi. Baada ya swala, Baraza la Eid litaendelea katika eneo hilo hilo.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk. Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana, ametumia nafasi hiyo kuwatakia Waislamu na Watanzania wote maandalizi mema ya kusherehekea Sikukuu hiyo kwa amani, mshikamano na kumcha Mwenyezi Mungu.