Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji alifanya ziara ya kujitambulisha kwa Balozi wa Uingereza nchini Msumbiji, Mhe Balozi Helen Lewis.

Katika Mazungumzo yao, Viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili (bilateral relations) na yale yalio chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Madola (commonwealth). Vilevile, walikubaliana kuendeleza uhusiano wa kihistoria sambamba na kuisaidia Msumbiji katika masuala ya kijamii, maendeleo na utunzaji wa amani na usalama, hasusan Kaskazini mwa nchi hiyo.

Mhe Balozi Hamad alitumia fursa hiyo kumuomba Mhe Balozi Lewis kuwashawishi wafanyabiashara wa Uingereza waliopo Msumbiji na maeneo mengine ya Kusini mwa Afrika kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania hasa kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo.

Aidha, alieleza mikakati inayofanywa na Ubalozi katika kubidhaisha Lugha ya Kiswahili ikiwemo kuanzisha mafunzo ya lugha hiyo kwa wafanyakaazi wa TV na Radio Msumbiji na kwamba hivi karibuni Ubalozi utaanzisha Kituo cha Utamaduni (Culture Centre) ambacho pamoja na malengo mengine, kitatumika pia kutoa mafunzo ya Lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Lewis aliahidi kutoa kila aina ya ushirikiano kwa Mhe. Balozi Hamad katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, alipongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania ikiwemo uimarishwaji wa huduma za kijamii, uboreshaji wa miundombinu na kuimarika kwa demokrasia. Alitumia nafasi hiyo kuitakia Tanzania kila la heri katika maandalizi ya Uchanguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba, 2025.