Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Dkt. Habib Kambanga, amekutana na kuukaribisha rasmi ujumbe wa Tanzania uliowasili jijini Kigali kushiriki Mkutano wa 16 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Rwanda, unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 hadi 26 Julai 2025.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania mjini Kigali, ambapo Mhe. Balozi Kambanga alipokea ujumbe huo na kuwakaribisha wajumbe hao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi Kambanga alieleza kuwa JPC ni jukwaa la kimkakati linaloimarisha ushirikiano wa kindugu kati ya Tanzania na Rwanda na kubainisha kuwa mikutano hiyo hutoa fursa ya kujadili kwa kina masuala ya maendeleo ya pamoja, kukuza ushirikiano wa karibu, na kuimarisha uhusiano katika sekta mbalimbali zikiwemo kijamii, kiuchumi, na kiusalama.

Balozi Kambanga aliwahimiza wajumbe hao kutumia fursa ya mkutano huo kubaini maeneo mapya ya ushirikiano, kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili, na kuhakikisha kuwa majadiliano yote yanazingatia maslahi mapana ya taifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Bujiku, alisisitiza umuhimu wa maandalizi ya kitaalamu, yenye weledi na uzalendo wa hali ya juu na kueleza kuwa hatua ya maandalizi inajumuisha kupitia misimamo ya Tanzania kuhusu masuala yanayotarajiwa kujadiliwa, pamoja na kuhakikisha kuwa taratibu zote muhimu zinakamilika kwa wakati ili kufanikisha mkutano kwa mafanikio makubwa.
Ujumbe wa Tanzania unajumuisha maafisa kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za serikali, pamoja na wataalamu na viongozi kutoka sekta tofauti. Miongoni mwa maeneo ya kipaumbele yatakayojadiliwa katika Mkutano wa 16 wa JPC ni pamoja na: Biashara na Viwanda, Miundombinu na Uchukuzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Ulinzi na Usalama, Utalii, Kilimo, Nishati, Elimu, na masuala ya kiuchumi kwa ujumla.
