Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Stephen Mbundi amekutana na Washiriki wa Kozi ya 14 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) waliotembelea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mtumba jijini Dodoma kwa ziara ya Mafunzo.
Akizungumza katika kikao na wanachuo hao Mhe. Balozi Mbundi alieleza kufurahishwa kwake na ziara hiyo ambayo inawapatia mafunzo kwa vitendo wanachuo hao na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, majadiliano ya kimkakati, na mbinu za pamoja kama nyenzo za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia.
Alisema kuwa mazingira ya usalama duniani yanabadilika kutokana na changamoto mbalimbali kama za mivutano ya kisiasa kati ya mataifa, uhalifu wa kuvuka mipaka, ugaidi, vitisho vya mtandao, mabadiliko ya tabianchi na za kiuchumi.
Aliongeza kuwa ni matumaini yake ziara hiyo itachangia kuimarisha uelewa wa washiriki kuhusu uhusiano kati ya diplomasia, usalama wa taifa na ushirikiano wa kimataifa na kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Mambop ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Chuo hicho.
Katika kikao hicho Balozi Mbundi alielezea kwa ufupi historia, majukumu, dira na dhamira ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kusimamia sera ya mambo ya nje, kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, na kukuza ushirikiano wa kikanda kupitia taasisi kama Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha NDC, Brigedia Jenerali Selemani Bakari Gwaya alieleza kuridhishwa kwao na mchango wa Wizara katika kufanikisha kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho ambao unakiwezesha kukua kimataifa na kuaminika kama taasisi ya kimkakati.
Amepongeza juhudi za Wizara kwa kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa weledi na Vitendo licha ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika siasa za kimataifa.
Wanachuo 72 wa Kozi ya 14 ya NDC kutoka nchi 17 za Tanzania, Bangladesh, Botswana, Burundi, Misri, Ethiopia,India, Kenya, Malawi, Namibia, Nigeria, Rwanda, Sierra Leone, Afrika Kusini, Uganda.







