Maboresho makubwa ya miundombinu yaliyotekelezwa na Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia Mradi wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP) yanaendelea kuzaa matunda, baada ya bandari hiyo kupokea meli kubwa na ndefu zaidi ya makasha kuwahi kutia nanga, yenye urefu wa meta 304.40.

Meli hiyo ya makasha, inayofahamika kwa jina la MSC STELLA, ina urefu unaolingana na viwanja vitatu vya mpira wa miguu vilivyopangwa mfululizo, tukio linalothibitisha hatua kubwa iliyofikiwa na Bandari ya Dar es Salaam katika kuongeza uwezo wake wa kuhudumia meli kubwa kwa viwango vya kimataifa.

MSC STELLA imewasili kutoka Bandari ya Jebel Ali, Dubai, moja ya bandari kubwa duniani. Ujio wake unaipa Bandari ya Dar es Salaam heshima kubwa, unaongeza kujiamini kiutendaji na kiusalama, na kuendelea kuipambanua bandari hiyo katika ramani ya usafirishaji wa kimataifa. Tukio hili pia ni uthibitisho wa moja kwa moja wa mafanikio ya uwekezaji wa Serikali kupitia Mradi wa DMGP, ulioboreshwa kwa kuongeza kina cha lango la kuingilia bandari, kuimarisha magati, kuboresha mifumo ya uratibu wa shughuli za kibandari na kuongeza ufanisi wa jumla wa utoaji huduma.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Meli na Uratibu wa Shughuli za Kibandari, Kapteni Abdullah Mwingamno, amesema ujio wa meli hiyo ni baraka na faida kubwa kwa Bandari ya Dar es Salaam, akieleza kuwa umewezekana kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali.

Kapteni Mwingamno ameeleza kuwa kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kupokea meli zenye urefu wa hadi meta 320, huku viwango vya juu vya kimataifa vikifikia takribani meta 405, hali inayothibitisha kuwa bandari hiyo inakaribia kwa kasi viwango vya dunia katika kuhudumia meli kubwa za kisasa.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yameongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa bandari, mapato ya Serikali na ubora wa huduma za shehena, na kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa chaguo la kuaminika kwa kampuni za usafirishaji wa kimataifa.

Kapteni Mwingamno ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika maboresho ya bandari nchini kote, akisema uwekezaji huo umeongeza ufanisi, kuimarisha ushindani wa kikanda na kuinua nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kupokelewa kwa meli hiyo kubwa ya makasha kutoka Jebel Ali ni ishara nyingine kwamba Bandari ya Dar es Salaam inaendelea kubadilika kutoka bandari ya kawaida kwenda bandari ya kisasa yenye uwezo wa kimataifa, tayari kushindana na bandari nyingine kubwa barani Afrika na duniani.