Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imesema imepiga hatua katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2024, huku ikitoa onyo kali kwa wasanii wanaotumia majukwaa yao kuhamasisha matumizi ya mihadarati kupitia maudhui ya nyimbo na mitindo ya mavazi.
Kauli hiyo imetolewa leo June 23 ,2025 Bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu William M. Lukuvi mara baada kuwasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2024, taarifa ambayo ni hitaji la kisheria chini ya Sheria ya mwaka 2015 inayohitaji tathmini ya kila mwaka kuhusu hali ya mapambano dhidi ya mihadarati.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uwasilishaji huo, Lukuvi amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendeleza mapambano dhidi ya mihadarati kwa kutumia mbinu shirikishi zinazohusisha mamlaka mbalimbali, Taasisi za ulinzi na usalama, jamii, sekta binafsi na wadau wa kimataifa.

Amesema kwa mwaka 2024, bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi ambapo Jumla ya tani 2,307.37 zilinaswa, kati ya hizo tani 2,303.2 zikitoka ndani ya nchi na tani 4.17 zikiwa ni Skanka kutoka mataifa ya Kusini mwa Afrika.
Amefafanua kuwa Skanka, ambayo ni bangi yenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC, iliongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka 2023, jambo linaloonesha kuimarika kwa udhibiti wa biashara haramu ya dawa hizo kupitia mipaka, viwanja vya ndege na bandari.
Pia ameeleza kuwa Serikali ilikamata tani 1.7 za methamphetamine, kilo 433.02 za heroin, gramu 853 za cocaine, na kwa mara ya kwanza kilo tano za dawa mpya aina ya Methylene-dioxy-pyrovalerone (MDPV).
Zaidi ya hayo, tani 18.45 za mirungi, kilo 56.78 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na tani 29.6 za kemikali bashirifu zilinaswa kwa usaidizi wa mifumo ya udhibiti wa kielektroniki.
Katika kusaidia waathirika wa dawa za kulevya amesema Serikali iliendelea kutoa tiba kwa waraibu kupitia vituo 16 vya methadone vilivyohudumia waraibu 17,975 na kwamba Nyumba 62 za upataji nafuu (sober houses) pia ziliendelea kutoa huduma kwa waraibu 17,230 waliotambuliwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Waziri Lukuvi ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa vitendo pamoja na wataalamu wa afya, mashirika ya kiraia, vyombo vya usalama, pamoja na wananchi kwa mshikamano wa pamoja uliosaidia kufanikisha mafanikio hayo.

Amesema, “Hili si tatizo la sekta moja. Linahusisha afya, usalama, elimu, ajira, na ustawi wa jamii,mafanikio ya kweli yanahitaji juhudi jumuishi kutoka serikalini, kwa wananchi, sekta binafsi na wadau wa kimataifa,” amesisitiza.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, ameonya vikali tabia inayoendelea kushika kasi miongoni mwa wasanii wanaotumia kazi zao kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema, “Tunaendelea kufuatilia kwa karibu nyimbo, video na mavazi yanayochochea utumiaji wa dawa za kulevya, Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa wote wanaopotosha jamii, hasa vijana,” amesema Kamishna Lyimo.
Amebainisha kuwa baadhi ya kazi za sanaa zimejaa maudhui ya kashfa, mavazi ya aibu na simulizi za kupambanua matumizi ya bangi na dawa nyingine hatarishi, hali inayochangia kuathiri maadili ya taifa na mapambano ya dawa hizo kwa ujumla.
“Sanaa si jukwaa la kutukuza mihadarati. Vijana wetu wanahitaji maudhui ya kuwajenga, si kuwaangamiza. Tutawachukulia hatua wote wanaokiuka sheria na taratibu za nchi,” ameongeza Lyimo kwa msisitizo.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mbinu za kiintelijensia, sheria na tiba katika kukabiliana na janga hili la kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuhimiza jamii kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapobaini au kushuku shughuli zinazohusiana na dawa za kulevya