Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwa kiungo muhimu katika kuwawezesha wakulima na wafugaji kufanikisha shughuli zao za kiuchumi kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara inayowaunganisha na masoko pamoja na huduma muhimu za kijamii.

Akizungumza jana katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Mhandisi Mshauri Pharles Ngeleja kutoka TARURA, amesema wakala huo umekasimiwa jukumu la kujenga na kukarabati mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 144,429.77 nchi nzima.

“TARURA katika maonesho haya inajitambulisha kama mshipa wa wakulima. Bila mishipa, huwezi kufika popote. Sisi ndiyo tunaowawezesha wakulima kufikisha mazao yao kwenye maeneo ya masoko,” amesema Mhandisi Ngeleja.

Amebainisha kuwa mtandao huo mkubwa wa barabara unahitaji ubunifu mkubwa hasa kwa maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi, huku akisisitiza kuwa barabara hizo ni lango la wakazi wa vijijini kufikia shule, hospitali, makanisa, misikiti na huduma nyingine muhimu.

Aidha, ametoa rai kwa wakulima na wafugaji kutunza miundombinu ya barabara inayojengwa na TARURA kwa kuwa ina mchango mkubwa katika ustawi wa shughuli zao za kila siku.

“Naomba wakulima na wafugaji waitunze na kuithamini miundombinu ya barabara tunayojenga vijijini kama ni ya kwao, kwa kuwa inalenga kuwawezesha wao moja kwa moja,” ameongeza.

Katika kuonesha ubunifu na ufanisi, Mhandisi Ngeleja amesema TARURA imekuwa ikitumia teknolojia mbadala inayozingatia mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo matumizi ya mawe katika ujenzi wa madaraja badala ya zege, hatua iliyosaidia kuokoa gharama kubwa.

“Kwa sasa tunatumia mawe katika ujenzi wa madaraja, ambayo ni nafuu zaidi kwa Wakala. Tangu kuanzishwa kwa TARURA, tumejenga madaraja 439 kwa gharama ya Shilingi bilioni 30,” ameeleza.

Amefafanua kuwa, endapo wangetumia teknolojia ya zege, gharama zingefikia zaidi ya Shilingi bilioni 103, lakini kupitia njia mbadala wameweza kuokoa fedha nyingi ambazo sasa zinaelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.

Amewakaribisha wananchi kutembelea banda la TARURA katika maonesho hayo ili kupata elimu na taarifa kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala huo katika kuboresha maisha ya wananchi wa mijini na vijijini kupitia miundombinu rafiki ya barabara.