Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imefanya kikao cha Baraza la madiwani , kikiambatana na zoezi la kuapisha kwa madiwani pamoja na uchaguzi Makamu Mwenyekiti wa baraza, chini ya Hakimu Gisella Jovinus Mangula.
Katika hotuba yake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Proscovia Mwamba, amewataka madiwani kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
“Ni wajibu wenu kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inasimamiwa kwa weledi na kwa maslahi ya wananchi,” amesema.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia utu na haki katika utoaji wa huduma Katika kuwahudumia wananchi, tuishi dhana ya utu na kutenda haki kwa kila mmoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Baraza la Madiwani, Sadoth J. Ijunga, ameishukuru CCM na madiwani wenzake kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo.
“Ninawashukuru kwa heshima hii. Nitaongoza kwa kushirikiana na madiwani wote na watumishi kuhakikisha shughuli za halmashauri zinafanyika kwa ufanisi,” amesema.
Ijunga pia ameongoza zoezi la kuunda kamati mbalimbali za baraza zitakazokuwa nguzo katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo ndani ya halmashauri.
Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza, ametumia kikao hicho kusisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa miradi na kutatua changamoto za wananchi.
“Madiwani lazima muwe mstari wa mbele kuzitatua changamoto za wananchi, hususan katika kupata huduma mbalimbali za kijamii,” amesema.
Ameongeza kuwa usimamizi bora wa miradi utapunguza kero zinazowakabili wananchi kila siku.
Baada ya kikao hicho, madiwani wote wamekabidhiwa vitendea kazi, huku wakitarajiwa kupatiwa mafunzo na semina mbalimbali zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu.





