Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BARAZA la Maaskofu katoliki nchini (TEC) limepiga marufuku viongozi wa kisiasa au kiserikali kupewa nafasi ya kuzungumza madhabahuni, iwe kusalimia, hotuba au kusema chochote.

Taarifa ya Mwongo wa Maboresho ya Liturujia iliyotolewa na baraza hilo ilieleza kuwa dhumuni kubwa ni kulipa heshima adhimisho hilo la ekaristi takatifu kama imani yao inavyowataka na si vinginevyo.

“Tumejikuta tumejenga tabia ya kuingiza matangazo mengi na hotuba nyingi kwenye maadhimisho mbalimbali ya kiliturujia, jambo hili likiachwa liendelee litafifisha heshima tunayopaswa kuitoa katika ukuu huo wa lituruji mbele ya Mungu wetu,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza utaratibu wa namna misa hiyo itakavyoendeshwa kwa kuainisha mpangilio wa namna ibada hizo zinavyotakiwa kuwa.

“Hakutakuwa na hotuba za kupongezana, isipokuwa tu mwadhimishi atatambua kwa ufupi uwepo wa wageni wa kidini, kiserikali, kijamii na waalikwa wote bila kuwapa nafasi ya kuongea, kutoa hotuba wala kusalimia,” ilieleza.

Iliongeza taarifa hiyo kuwa mwadhimishi mkuu ndiye atakayewajibika kuwaalika wageni kutoa zawadi zao bila ya wao kutoa salamu za pongezi.