Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media, Nzega

Mgombea ubunge Jimbo la Nzega Mjini Hussein Bashe, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuzingatia ombi la muda mrefu la kuugawa Mkoa wa Tabora.

Amesema hatua hiyo inatokana na wananchi wake kutembea umbali wa kilomita 220 kwenda kupata huduma mbalimbali.

Amesema mkoa mpya utasaidia kuhudumia wananchi wa Nzega, Igunga, Manonga, na Uyui Kaskazini ambao wamekuwa na shauku ya mrefu ya kupata mkoa.

Akizungumza na maefu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Samora mjini Nzega, Bashe amesema mkoa wa Tabora ni mkubwa kiutawala na wananchi wa maeneo ya mbali kama Bukene hulazimika kusafiri zaidi ya kilomita 220 kufuata huduma za mkoa.

“Tunakuomba Mkoa wa Nzega. Ukichukua Igunga, Manonga, Nzega DC na Uyui Kaskazini, watu ni zaidi ya milioni 1.8.

Tunaomba mkoa huu ugawanywe kwa sababu ni mkubwa mno. Ombi hili tumelilia kwa muda mrefu na litakuwa kumbukumbu kwako, Mama Samia,” alisema Bashe.

Bashe pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo vijijini, hasa katika sekta ya maji, elimu, umeme na miundombinu.

Alisema kata zote 10, vijiji 21 na vitongoji 176 vya Nzega Mjini sasa vina huduma ya maji safi na salama.

Pia zaidi ya Kaya 14,000 zimeunganishiwa maji kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.

“Wakati anaingia madarakani, kulikuwa na sekondari nne tu, lakini sasa zimefikia 16, na hakuna kata isiyo na shule ya sekondari.Kata zote zina umeme.Urefu wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 160 hadi 517.

Pia alisema barabara ya kutoka Kitangiri hadi Mwanayagula imejengwa, ikirahisisha usafiri na biashara kwa wakazi wa vijijini.

Katika sekta ya kilimo, Bashe alisema Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kusaidia wakulima.

Alisema msimu wa tumbaku umemalizika kwa mafanikio, huku wakulima wakipata ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 13.

“Hoja si kwamba atashinda au la, bali asilimia ya ushiriki wa wananchi ni muhimu. Tumejiwekea lengo la kufikia asilimia 90 hadi 95 ya ushiriki. Hii ni kazi ya wananchi,” alisema.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kumwamini na kumpa nafasi ya uongozi serikalini.

“Nashukuru sana umeniteua kuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri. Nakuhakikishia utii, uaminifu usio na kikomo, na nitatumikia nafasi hii kwa moyo wote na kwa wivu mkubwa,” alisisitiza Bashe.

Mwisho