Na Farida Mangube, Morogoro

Watu kumi wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo Januari Mosi 2026 katika eneo la Mwidu Mikese, mkoani Morogoro.

Ajali hiyo ilihusisha basi dogo na lori la mizigo imetokea katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Wilaya ya Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro ajali hiyo imetokea baada ya basi dogo lenye namba za usajili T 162 DMD, lililokuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Sherehe Juma, kugongana na lori la mizigo aina ya HOWO lenye namba za usajili T 956 ELU na tela namba T 828 ELW.

Lori hilo ni mali ya Kikori Company, lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Abuu mkazi wa Msoga Chalinze, mwenye umri kati ya miaka 26 hadi 28.

Dereva huyo alikuwa akisafirisha shehena ya mbolea kutoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya.

Majeruhi wote 18 wamekimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu, ambapo hali zao zinaendelea kufuatiliwa na wataalamu wa afya.

Jeshi la Polisi limethibitisha vifo hivyo na kueleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, huku likitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazogharimu maisha ya watu.