Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za mafuta zinazotumika kuanzia leo Septemba 3, 2025, zikionesha kupungua kwa kwa shilingi 36 kwa bei ya petroli na shilingi 23 kwa bei ya dizeli kwa mafuta yaliyopokelewa bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara mtawalia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Andilile, bei ya petroli katika soko la dunia imepungua kwa asilimia 0.2 %, dizeli kwa 5.5 % na mafuta ya taa kwa 3.5%. Vilevile, kwa bei za mwezi Septemba, 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa 3.96%

Gharama za kuagiza mafuta katika Bandari ya Dar es salaam zimeongezeka kwa wastani wa 20.73% kwa mafuta ya petroli, 7.75% kwa mafuta ya dizeli na 2.62% kwa mafuta ya taa; katika Bandari ya Mtwara hakuna mabadiliko, na kwa Bandari ya Tanga zimepungua kwa 12.66% kwa mafuta ya petroli na 12.66% kwa mafuta ya dizeli.

Aidha, wafanyabiashara wanakumbushwa kuuza mafuta kwa bei zilizoidhinishwa na EWURA na yeyote atakayekiuka agizo hili atachukuliwa hatua kali za kisheria.