Bei ya mafuta imeshuka kwa karibu 5% Jumanne baada ya Israel kukubali kusitisha mapigano kati yake na Iran yaliyoendelea kwa karibu wiki mbili.
Bei ya kimataifa ya mafuta ghafi ya Brent ilishuka hadi $68 kwa pipa ilakini ikaimarika baada ya Iran na Israel kulaumiana kwa kukiuka makubaliano ya usitishaji mapigano ndani ya saa chache.
Bei ya mafuta ilipanda katika siku za hivi karibuni huku wasiwasi ukiongezeka kwamba Tehran inaweza kuvuruga shughuli ya usambazaji wa mafuta kimataifa kwa kuziba Mkondo wa Bahari wa Hormuz, njia kuu ya usafirishaji wa mafuta na gesi.
Masoko ya hisa nchini Marekani, Uingereza na Ulaya yalipanda na kuimarika baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuiambia Israel kwenye mitandao ya kijamii isirushe mabomu baada ya kuishutumu Iran kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
