Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
BENKI ya Ushirika (Coop Benki), kwa kushirikiana na Mfuko wa Pembejeo wa Kilimo (AGITIF), imetoa mkopo wa Shilingi bilioni 8.5 kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika, ikiwa ni hatua ya kuchochea kilimo chenye tija na kuwainua vijana pamoja na wanawake waliopo katika sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Benki, Godfrey Ng’urah, alisema mikopo hiyo inalenga kuimarisha uzalishaji mashambani na kufungua fursa zaidi kwa wakulima, hasa walioko vijijini.
“Benki ya Ushirika inashirikiana na AGITIF kutoa mikopo kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika, ikiwa ni pamoja na vijana na wanawake. Leo tunatoa mkopo wa dhamani ya shilingi bilioni 8.5 kwa dhamira ya kuchochea kilimo chenye tija,” alisema Ng’urah.
Alifafanua kuwa Mfuko wa AGITIF, ambao ulianzishwa mwaka 1994, una lengo la kutoa huduma za kifedha kwa watu binafsi katika sekta ya kilimo, taasisi za kifedha pamoja na makundi maalum ya kijamii.
“Mfuko huu umeelekeza nguvu kubwa kwa vijana walio na umri chini ya miaka 40 pamoja na wanawake, kwa kuwa ni makundi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kilimo,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Ng’urah, hadi sasa AGITIF imeshatoa zaidi ya Shilingi bilioni 94 zilizowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji na kuongeza uzalishaji mashambani kote nchini.
Alisisitiza kuwa Coop Benki itatekeleza jukumu la kuwa wakala wa mikopo hiyo, ikitumia mtandao wa vyama vya ushirika na matawi yake yote ili kuwafikia wakulima kwa urahisi, mijini na vijijini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar, aliwahimiza wakulima kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuongeza mzunguko wa fedha na kuwezesha wakulima wengine kunufaika.
“Tunatoa wito kwa wakulima wanaokopeshwa kuhakikisha wanarejesha mikopo hii kwa wakati. Hii itawezesha wengine pia kupata fursa sawa ya kuendeleza shughuli zao za kilimo,” alisema Dkt. Hussein.
Mpango huu unakwenda sambamba na juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo kupitia upatikanaji wa mitaji nafuu, kuongeza tija, kipato cha kaya pamoja na kuchochea ajira katika maeneo ya vijijini.
