Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Matavila, ameishukuru Benki ya Dunia kwa msaada wa kifedha na kitaaluma wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Akifungua kikao cha Kamati Kuu (National Steering Committee) ya Usimamizi wa Mradi wa Kujenga Ustahimilivu wa Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (SCALE), mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam, kama Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, Mhandisi Matavila alisema, kikao hicho ni muhimu kwakuwa kinatoa fursa ya kuanza utekelezaji kwa vitendo baada ya kupitia ripoti za halmashauri zote 65 ambazo zitawasilishwa Benki ya Dunia ili kuwezesha kutolewa kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya hatua ya awali ya utekelezaji.
Mradi wa SCALE unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatarajiwa kufikia wananchi zaidi ya milioni 6.6 katika kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia 2025 hadi 2030. Mradi huo utatekelezwa katika halmashauri 65, zikiwemo 54 za Tanzania Bara na 11 za Zanzibar.
Benki ya Dunia imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua nzuri iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa Kujenga Ustahimilivu wa Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (SCALE).
Akizungumza katika kikao hicho, mwakilishi wa Benki ya Dunia na mshauri wa mradi wa SCALE, Dkt. Lucy Ssendi, amesema mradi huo umeonyesha mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu kuanza kwake. Ameeleza kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza mwishoni mwa mwaka jana, Serikali imechukua hatua za kuimarisha utekelezaji na sasa hali inaendelea vizuri
Dkt. Ssendi ameshukuru Serikali pamoja na sekta zake kwa kujitolea kuhakikisha utekelezaji wa mradi unaendelea hata kabla ya kupokea fedha. Amesisitiza kuwa Benki ya Dunia inathamini ushirikiano uliooneshwa na Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar katika kusimamia na kuendeleza mradi huo.
Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa mradi huo, Bi.Hawa Mwechanga, alisema mradi wa SCALE unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani Milioni 110, ambapo asilimia 90 ya fedha zitaelekezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na asilimia 10 kubaki Serikali kuu kwa ajili ya uratibu na usimamizi wa mradi.





