*GBT yasema burudika kwa kiasi, ukishiriki sana utaingia kwenye uraibu

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), Daniel Ole Sumayan, amesisitiza umuhimu wa waendesha michezo hiyo kuzingatia matakwa ya kisheria ili kuhakikisha sekta inabaki salama na yenye kuchochea uchumi.

Sumayan amesema kuwa uchangiaji umeongezeka kutoka Sh.Bilioni 131.99 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Bilioni 260.1 kwa mwaka 2024/25 ambapo ongezeko hilo la kiasi cha fedha linatajwa kufikia asilimia 97.

Akizungumza katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kilichoandaliwa na Msajili wa Hazina Bw. Sumayan kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe, amesema kuwa kuna mafanikio makubwa ya bodi hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) Olesumayan Daniel akizungumza kuhusiana na mafanikio ya Bodi katika kipindi cha awamu ya Sita ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa mbali ya ongezeko hilo na kuchangia kodi pia imefanikiwa kutoa ajira 30,000 ambazo ni rasmi na zisizo rasmi.

“Mafanikio mengine ni pamoja na zaidi ya Sh.Bilioni 66.7 kuingizwa nchini kutoka kwa wawekezaji wapya kwa kipindi cha miaka miwili Bodi hiyo imewezesha kukusanya kwa fedha ndogo ndogo na kuifanya kuwa mitaji mikubwa iwezayo kuwekeza jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limechangamsha uchumi wetu.” amesema Naibu Mkurugenzi Ole Sumayan.

Ameongeza kuwa Ole Sumayan amebainisha kuwa Bodi imewezesha kuchangia Sh.Bilioni .53.8 kwa ajili ya kuendeleza michezo nchini.

Amesema kuwa mifumo ya michezo ya kubahatisha hutumia vifaa na mashine mbalimbali, na Bodi huweka viwango vya kiufundi ili kuhakikisha michezo inaendeshwa kwa usawa bila udanganyifu na ikiwa chini ya sheria.

Hata hivyo amesema kuwa michezo ya kubahatisha ni burudani, lakini inapozidi mipaka inaweza kusababisha matatizo. Hivyo, ni muhimu kuhimiza ‘Responsible Play au Responsible Gaming’ kucheza kwa kiasi na kuondoka wakati bado kuna ladha ya burudani ili kuepuka uraibu.

“Dhana inayotawala ushiriki katika michezo ya kubahatisha ni bahati na burudani. Lengo la kucheza ni burudani; sio ajira. Michezo hiyo ikiwemo ya kubashiri matokeo ya soka ni sehemu ya kuongeza wigo wa urudani kwa wachezaji kama ilivyo wapenzi wa soka na michezo mingine.Kupata kuna burudani yake na kukosa kuna burudani yake. Watu wetu wabebe hiyo kwamba hii ni burudani na kushinda ni bahati tu.

“Burudika kwa kiasi. Burudika bado ikiwa tamu, usiondoke ikiwa chungu. Maana ukishiriki sana utapata shida, utaingia kwenye uraibu. Hatutaki ilete kero, tunataka iwe burudani,” amefafanua Ole Sumaiyan

Bodi ina jukumu la kulinda jamii dhidi ya madhara yatokanayo na michezo hiyo, ikiwemo uraibu, na kutatua migogoro kati ya wachezaji na waendeshaji inapojitokeza.

Pia imeeleza kuwa kuna aina mbili za michezo ya kubahatisha ya kibiashara inayohusisha uwekezaji wa makampuni kama kasino na michezo ya mtandaoni na isiyo ya kibiashara inayolenga maendeleo ya jamii.

Akifafanua zaidi, ameeleza tofauti kati ya kasino na vilabu vya burudani kama night clubs, akibainisha kuwa kasino zinajumuisha slot machines na meza za michezo maalum. Aidha, teknolojia imewezesha uwepo wa kasino za mtandaoni ambazo zina taratibu maalum za uendeshaji.

“Bodi hutoa leseni kwa waendeshaji na maeneo yanayowekwa mashine hizo, ikiwa ni pamoja na maduka yenye mashine zisizozidi 40, bahati nasibu ya taifa na michezo mingine. Bahati nasibu ya taifa, ambayo ni mali ya Serikali, huendeshwa na sekta binafsi kupitia leseni maalum, na mapato yake huchangia maendeleo ya michezo nchini kupitia Baraza la Michezo la Taifa” amesema.

Pia, ameeleza kuwa kuna michezo inayotumika kama nyenzo ya kutangaza biashara, ambapo washiriki hupata zawadi kama bidhaa, fedha au huduma. Hata hivyo, ameonya kuwa ni kinyume cha sheria kuendesha michezo ya kubahatisha bila leseni kutoka Bodi.

Amesema changamoto zilizokuwepo awali, ambapo mamlaka nyingine zilikuwa zikitoa vibali bila kushirikiana na Bodi, zimepungua kupitia elimu kwa umma.

Leseni hutolewa kwa mwaka mmoja na huhuishwa endapo mmiliki atazingatia vigezo, ikiwemo kutoshirikisha watoto. Michezo hiyo hairuhusiwi kuendeshwa karibu na nyumba za ibada, shule au maeneo ya usalama.

Ameongeza kuwa maeneo yasiyo na leseni au yanayowawezesha watoto kushiriki hayajaidhinishwa na Bodi, na ukaguzi wa maeneo ni sehemu ya mchakato wa utoaji leseni.

Amewahimiza waandishi wa habari kutembelea kasino ili kupata uelewa wa moja kwa moja, akisema, “Kuona ndiyo kuamini”, na kwamba uelewa huo utawawezesha kuripoti kwa usahihi na mamlaka.