Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Karagwe

Wananchi zaidi ya 100,000 wameanza kunufaika na biashara ya kaboni kupitia mradi wa kilimo mseto unaotekelezwa katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange wilayani humo.

Akizungumza na wananchi alipotembelea na kukagua mradi kilimo mseto (Kinoni Agroforestry Farm) unaotekelezwa na Kampuni ya KADERES, Dkt. Dugange alisema eneo la utunzaji wa mazingira limepewa kipaumbele.

Alisema Serikali imedhamiria kuwainua wananchi wake kwa kujenga uchumi na kukikisha wanatumia fursa ya biashara ya kaboni ili mwananchi mmoja mmoja anufake.

“Nimeona shamba hili zuri lina miaka kadhaa na tumepata taarifa hapa lengo ni kuhakikisha wananchi hadi milionimoja wananufaika na biahasra ya kaboni kupitia mashamba yao hii ni habari njema sana maana pamoja na kuvuna mazao yenu kama migomba, kahawa mnanufaika na biashara ya kaboni,“ alisema.

Aidha, Dkt. Dugange pamoja na kuupongeza uongozi wa mkoa, wilaya na kampuni hiyo, pia alitoa wito kwa wananchi wachangamkie fursa hiyo na kujisajili ili ili waingie katika mfumo rasmi na hatimaye kunufaika na fedha hivyo kujikwamua kiuchumi.

Aliongeza kuwa tayari Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuwaunga mkono ikiwemo kutoa elimu kuhusu namna bora ya kuhifadhi mazingira ili kuendelea kunufaika.

Halikadhalika, Naibu Waziri huyo alisema kuwa kupitia Bunge limepitisha sheria sheria ya kuanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) ambacho kinawezesha usajili wa miradi ya biashara hiyo nchini.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Kampuni ya KADERES Bw. Leonard Faustine aliishukuru Serikali kwa kuwa nao bega kwa bega kwa kuwapa ushirikano katika utekelezaji wa mradi huo.

Alisema ushiriki wa Serikali kwenye mikutano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi imeleta tija katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili nchi.