Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma
MKUU WA WILAYA ya Tunduru Simon Chacha,amepongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji(NIRC), kwa uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 3 kwaajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya Umwagiliaji katika skimu ya Mkotamo, wilayani Tunduru
Mradi huu unatarajiwa kunufaisha wakulima zaidi ya 497, kwa kulima eneo lenye ukubwa wa ekari 867 kwa kilimo cha mpunga na mbogamboga.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini ya ujenzi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha alisema:
“Kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa wilaya yetu, hivyo serikali imewekeza katika miradi hii ili kuhakikisha wakulima wanapata msaada wa maji wa uhakika”,
Aidha, alibainisha kuwa skimu hii itawapa wakulima uwezo wa kulima mazao kwa mwaka mzima bila kutegemea mvua na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao
Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Ruvuma, Lucia Chaula, ameongeza kuwa skimu hiyo inalenga kuimarisha kilimo endelevu kwa kulinda rasilimali za maji na mazingira.

“Mradi huu siyo tu unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao, bali pia unaleta maendeleo endelevu kwa kuhakikisha rasilimali za maji na mazingira vinahifadhiwa kwa jitihada za pamoja”, amesema
Mhandisi Chaula ameongeza kuwa Mradi huo, unaotarajiwa kutekelezwa ndani ya miezi 12 kuanzia Aprili , 2025 hadi Aprili 2026 na kwamba unahusisha ujenzi wa banio, mifereji mikuu na midogo, barabara za mashambani, pamoja na vivuko vya maji ili kurahisisha usafiri wa wakulima.
Ujenzi wa Miundo mbinu katika skimu ya Mkotamo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita, kufanikisha kilimo chenye tija, kupitia kilimo cha Umwagiliaji



