Na Dk. Reubeni Lumbagala, JamhuriMedia, Tanga
Elimu ni gharama. Wahenga wakaweka wazi ukweli huu kwa kusema “Ikiwa unaona elimu ni ghali, basi jaribu ujinga.” Ni ukweli ulio dhahiri kuwa gharama za kupata elimu ziko juu, ndiyo maana serikali ikachukua jukumu la kuja na kutekeleza kwa vitendo Sera ya Elimumsingi Bila Ada kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Sita. Hili limefanyika kwa lengo la kuwapunguzia wazazi na walezi mzigo mkubwa wa gharama za kugharamia elimu za watoto na ndugu zao.
Serikali sasa inatoa Ruzuku ya Uendeshaji (Capitation Grants) kwa shule zake zote za msingi na sekondari ili kufanikisha shughuli za taaluma, utawala, mitihani, michezo, ukarabati na shughuli nyinginezo ndogondogo katika ngazi ya shule.

Kwa upande wa elimu ya kati na ya juu, serikali inatoa mikopo kwa wanafunzi kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili waweze kumudu gharama za elimu na hatimaye waweze kutimiza ndoto zao za kupata elimu ya juu na hatimaye waweze kujiajiri au kuajiriwa na hatimaye wajenge maisha yao na nchi yao kwa ujumla.
Kutokana na mafanikio makubwa katika maboresho ya sekta ya elimu, kumekuwa na ongezeko la waombaji mikopo ya elimu ya kati na ya juu kila mwaka. Hii imepelekea serikali kuiongeza bajeti HESLB kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya waombaji wenye sifa ambao kwa kweli ni wengi sana.
Kwa mfano, kwa mwaka wa masomo 2024/2025, serikali iliidhinisha Shilingi Bilioni 787 zitumike kuwakopesha wanafunzi. Aidha, kwa mwaka 2025/2026, Shilingi Bilioni 916.7 zinatarajiwa kutumika kwa wanufaika 252,773. Haya ni mageuzi makubwa yamefanyika ili kuhakikisha kila kijana wa Kitanzania anapata haki ya elimu.

WAOMBAJI MIKOPO SOMENI MIONGOZO KABLA YA KUOMBA.
Umekuwa ni utaratibu wa HESLB kutoa miongozo ya uombaji mikopo na ruzuku kila mwaka kabla ya kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya mikopo. Lengo la kufanya hivi ni kuwapa waombaji uelewa wa pamoja wa vitu vya msingi vya kuzingatia kabla ya kuomba ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata mikopo kwani kwenda kinyume na mahitaji ya miongozo, ni kujiweka katika mazingira ya kukosa mikopo.
Juni 6, 2025 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo alizindua miongozo ambapo amewasihi wanafunzi, wazazi na walezi kusoma miongozo hiyo kabla ya kuomba mikopo ambapo dirisha la uombaji mikopo litafunguliwa rasmi Juni 15, 2025 hadi Agosti 31, 2025.
“Katika mwaka mpya wa masomo 2025/2026 utakaoanza Oktoba 2025, bajeti iliyoidhinishwa ni Shilingi 916.7 Bilioni ambayo imeongeza idadi ya wanufaika kutoka 145,000 mwaka 2021 hadi wanufaika 252,773 mwaka 2025/2026 kati ya idadi hiyo, wanafunzi 88,320 watakuwa wa mwaka wa kwanza, wakiwemo wanafunzi wapya wa stashahada, wanafunzi wa shahada za awali, wanafunzi wa stashahada ya juu ya mafunzo ya sheria kwa vitendo, wanafunzi shahada za juu na Samia Skolashipu,” amesema Prof. Nombo.
Niwakumbushe tena waombaji mikopo kuisoma kikamilifu miongozo yote ya uombaji mikopo na ruzuku iliyotolewa na HESLB ili kuzingatia vitu vya msingi kabla hawajaomba mikopo hiyo. Miongozo hiyo inahusisha mikopo kwa stashahada (Diploma), mikopo kwa shahada ya awali (Bachelor degree).

Vilevile, mikopo ya stashahada ya juu ya sheria kwa vitendo, mikopo ya shahada za uzamili na uzamivu (Master and PhD) na Ruzuku (Samia Scholarships). Ikumbukwe kuwa serikali kwa upande wake imeshawekeza Bilioni 916.7 tayari kwa matumizi kwa waombaji wenye vigezo na wale wanaoendelea na masomo. Kazi kwenu vijana, kuchangamkia fursa hii.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga na Naibu Afisa Habari wa Jukwaa la Wazalendo Huru Tanzania.
Maoni: 0620 800 462