Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

BONDIA Abdul Zugo wa Tabora amempiga kwa KO raundi ya tatu bondia Sameer Kumar kutoka India na kuvishwa Mkanda wa Ubingwa wa Dunia wa Uzito wa Kati katika pambano la Kimataifa lililoandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani (WPBF).

Pambano hilo la raundi 10 limepigwa juzi katika ukumbi wa Orion Hotel Mjini Tabora na kushuhudiwa na umati mkubwa wa wapenzi wa masumbwi kutoka Wilaya zote za Mkoa huo na Mikoa jirani na wadau mbalimbali.

Akicheza kwa umakini mkubwa na kujiamini bondia Zugo amembana mpinzani wake kuanzia raundi ya kwanza huku akimpiga ngumi nzito za kushtukiza usoni ambazo zilimfanya mpinzani wake kukosa mwelekeo na kushindwa kujilinda.

Katika dakika ya pili ya raundi ya tatu, Zugo aliachia ngumi nzito iliyotua usoni kwa mpinzani wake na kuanza kutokwa na damu puani, hali iliyomfanya ajisikie vibaya na kuinama, mwamuzi akahesabu hadi kumi na kuhitimisha pambano.

Akiongea baada ya kuvishwa mkanda wa ubingwa huo, Zugo amewashukuru mashabiki wake na Uongozi wa Mkoa kwa kumpa sapoti kubwa wakati wa maandalizi yake, alibainisha kuwa ushindi huo ni wa wana Tabora wote.

Awali katika mapambano 14 ya utangulizi bondia Karim Mandonga (mtu kazi) amepokea kichapo kutoka kwa bondia Juma Farahan wa Tabora katika pambano la raundi 4, Farahan ameshinda kwa pointi.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella amempongeza kwa ustadi wake katika mchezo huo na kumhakikishia kuwa serikali ya Mkoa itaendelea kumuunga mkono.

Amewataka wanamichezo, viongozi na wadau wote wa michezo katika Mkoa huo kuendelea kushikamana ili kuinua vipaji vingi vya wanamichezo ili mkoa huo uendelea kutangazwa vizuri kupitia michezo.