Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

NYOTA ya Bondia wa Kimataifa, Mtanzania Abdul Zugo kutoka Tabora imeendelea kung’ara katika mapambano mbalimbali aliyocheza hivi karibuni ndani na nje ya nchi na sasa anajiandaa kuwania ubingwa wa dunia wa uzito wa kati.

Akizungumza na vyombo vya habari jana mjini hapa bondia Zugo ameeleza kuwa kiwango chake sasa hivi kiko juu sana kwani katika mapambano 18 aliyocheza ndani na nje ya nchi ameshinda mapambano 15, KO 13, sare 2 na kupoteza 1.

‘Naushukuru sana Uongozi wa Mkoa wa Tabora chini ya Mkuu wa Mkoa Paul Chacha kwa sapoti kubwa wanayonipa ambayo imeniwezesha kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kila pambano ninalocheza, sasa hivi niko vizuri sana,’amesema.

Zugo amebainisha kuwa baada ya kucheza mapambano 2 ya kimataifa nje ya nchi na kufanya vizuri, sasa anajiandaa kupanda ulingoni Agosti 23 mwaka huu katika pambano la ubingwa wa dunia la uzito wa Super Light Weight kg 63.

‘Natarajia kupambana na bondia Rajesh Kumar kutoka India katika pambano la ubingwa wa dunia linaloandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani (WPBF), litakalofanyika Tabora, nitaonesha knockout ya Mama,’ ameeleza.

‘Naomba wadau mbalimbali wakiwemo Azam wajitokee kunidhamini katika pambano hili na mengine yajayo ili niendelee kufanya vizuri zaidi na kuheshimisha nchi yetu’, ameomba Bondia Zugo.

Akizungumzia pambano hilo, Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha amempongeza Kijana Zugo kwa umahiri wake na kuendelea kujituma zaidi katika mazoezi yake hali ambayo imemfanya kuwa miongoni mwa mabondia bora hapa nchini.

‘Kijana wetu anafanya vizuri sana, tutaendelea kumpa ushirikiano na kila msaada atakaohitaji ili aendelee kupeperusha vyema bendera ya Tanzania na kuutangaza Mkoa wa Tabora kila anakoenda, tunataka Agosti 23 apige knockout ,’ amesema.