BOT, Wadau Kimataifa waipongeza Benki ya CRDB Mageuzi ya Mfumo Mkuu

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, amepongeza mageuzi ya kihistoria yaliyofanywa na Benki ya CRDB katika mfumo wake mkuu wa kibenki (core banking system), akisema ni hatua ya kimkakati inayoonesha ukomavu na uimara wa sekta ya benki nchini.

Tutuba alitoa pongezi hizo katika mkutano maalum kati ya menejimenti ya Benki ya CRDB na Benki Kuu uliofanyika jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa pia na Manaibu Gavana pamoja na Wakurugenzi wa BOT.

Pongezi za BOT zimekuja siku chache baada ya jumuiya ya kimataifa kuisifu Benki ya CRDB kwa mageuzi hayo, yaliyolenga kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha usalama wa miamala na kupanua huduma bunifu kwa wateja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 2, 2025, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema pongezi hizo zinadhihirisha imani ya wadau wa sekta ya fedha kwa benki hiyo na nafasi yake kama kinara wa ubunifu wa kidijitali barani Afrika.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akielezea utekelezaji wa mageuzi ya mfumo mkuu wa benki hiyo na nafasi yake katika kuboresha huduma, kuongeza usalama wa miamala na kufungua fursa mpya za kibiashara. Wengine pichani ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Emmanuel Kiondo (kushoto), na Meneja Mwandamizi wa Mahusiano kwa Umma, Kilo Mgaya.

“Hakuna safari ya mageuzi iliyo rahisi. Ni kweli baadhi ya wateja walipata changamoto za muda mfupi, lakini timu yetu ilifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kwa haraka. Sasa huduma zetu zimerudi kawaida na mageuzi haya yameweka msingi thabiti wa kutoa huduma Tanzania, Burundi, DRC, Dubai na masoko mapya tunayoelekea,” amesema Mwambapa.

Tully amefafanua kuwa mageuzi hayo ya mfumo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Muda wa Kati wa Benki ya CRDB (2023–2027), ambao unaweka ubunifu wa kiteknolojia kama msingi wa ukuaji wa benki na uchumi. Mageuzi haya pia yanaonesha ustahimilivu wa benki kwa kusimamia mabadiliko makubwa katika nchi tatu (Tanzania, Burundi na DRC) huku huduma zikiendelea bila kukatika, jambo lililopongezwa na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa, mageuzi hayo yamefungua milango ya ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo makubaliano yaliyosainiwa hivi kando ya mkutano wa UNGA na Shirika la Crop Trust kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula kupitia kilimo stahimilivu, na makubaliano na shirika la fedha la DIFC kwa ajili ya uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo na wakati.

Aidha, amesema Benki hiyo imesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiteknolojia na kampuni ya kimataifa ya teknolojia Huawei kwa ajili ya kuimarisha mabadiliko ya kidijitali, usalama wa mifumo na matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence).

“Ushirikiano huu ni wa kimkakati na utafungua fursa kubwa kwa wakulima wadogo kupitia teknolojia za kilimo stahimilivu, kwa wafanyabiashara kupitia huduma za kifedha zilizo salama zaidi, na kwa sekta za maendeleo kupitia ubunifu wa kidijitali na akili mnemba. Ni hatua inayoongeza ushindani wa uchumi wetu kikanda na kimataifa,” amesema Tully.

Vilevile, amesema mfumo huo mpya umeongeza uwezo wa benki hiyo kutoa huduma kwa viwango vya kimataifa kwa wateja binafsi, wafanyabiashara na makampuni, ndani ya Tanzania, Burundi na DRC, huku ukiweka mazingira thabiti ya upanuzi katika masoko mapya duniani.

“Kama mnavyotambua hivi karibuni tumepata kibali cha kufungua ofisi yetu huko Dubai, hatua ambayo inathibitisha nafasi ya Benki ya CRDB kama daraja kati ya Afrika na masoko ya kimataifa. Hii ni hatua ya kimkakati ya kuwaunganisha wateja wetu na mitaji, teknolojia na fursa mpya zinazopatikana katika masoko ya kimataifa,” ameongeza Mwambapa.

Amesema pamoja na pongezi hizo za kimataifa, Benki ya CRDB inatambua wajibu wake wa kuendelea kuboresha huduma, kuwekeza katika ubunifu na kuhakikisha kila hatua inayopiga inaleta mageuzi chanya katika maisha ya wateja wake na kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Mageuzi ya mfumo si tu yanadhihirisha uthubutu wa benki, bali pia ni ishara ya uimara na uthabiti wake katika kuhimili changamoto na kuendelea kusonga mbele kwa kujiamini,” amesema.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alialikwa kushiriki katika Kongamano la Biashara kati ya Marekani na Afrika (US–Africa Business Forum) lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York.

Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, mageuzi ya mfumo mkuu wa kibenki yaliyofanywa na Benki ya CRDB yalitambuliwa kama mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani.

Aidha, vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa ikiwemo Bloomberg vilimualika Nsekela kuelezea mageuzi hayo, ambapo mahojiano hayo yalitoa fursa ya kuonesha namna Benki ya CRDB inavyotumia teknolojia kuboresha huduma, kuongeza usalama wa kifedha na kuwezesha maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi barani Afrika. Hii imeifanya Benki ya CRDB kuwa miongoni mwa benki chache barani Afrika zinazotajwa kwa uwekezaji madhubuti wa teknolojia katika majukwaa makubwa ya kiuchumi duniani.

Mageuzi hayo pia yamepongezwa na wadau mbalimbali ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, alisema mageuzi hayo yametoa mfano wa uongozi wa kijasiri na yameongeza kujiamini kwa sekta ya fedha nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, aliyatambua mageuzi hayo kama mabadiliko ya kimkakati yanayodhihirisha uwezo wa Tanzania kuendesha mageuzi makubwa ya kidijitali kwa ufanisi mkubwa na salama. Wataalamu wa ndani wa TEHAMA, akiwemo Nguvu Kamando wa Vodacom, waliongeza kuwa mageuzi haya yanaweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa kama kiongozi wa ubunifu wa kifedha.