Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wabunge, Viongozi wa Serikali, Mashirika binafsi na wananchi wameungana jijini Dodoma katika kilele cha Bonanza Maalum la Bunge maarufu kama Grand Bunge Bonanza ambalo kwa mwaka huu limefanyika kama tukio la mwisho kwa Bunge la 12.

Bonanza hilo lilibeba kaulimbiu ya mwaka huu “Michezo kwa Afya, Umoja na Maendeleo” limehusisha mashindano mbalimbali yakiwemo mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba na riadha.

Akizungumza kwenye bonanza hilo leo June 21,2025 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa asisitiza kuwa michezo ni nguzo muhimu ya kuimarisha afya, mshikamano na maendeleo ya taifa.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Bunge katika kuendeleza jitihada hizo.

“Kwa miaka mitano mfululizo Grand Bunge Bonanza limekuwa jukwaa la kuhamasisha mazoezi na maisha bora,faida zake ni pana kutoka kwa wabunge, wafanyakazi wa Bunge hadi kwa wananchi wa kawaida,” amesema Majaliwa.

Mwenyekiti wa Bonanza hilo, ambaye pia ni Mbunge wa Makete, Festo Sanga, ameishukuru Serikali na wadau kwa kuendelea kuunga mkono shughuli za michezo, akisema kuwa mbali na kuchangia afya, michezo ni nyenzo ya kujenga ajira na mshikamano wa kitaifa.

“Bonanza hili limekuwa chachu ya mshikamano, afya ya mwili na akili, na hata kutengeneza marafiki kati ya wabunge, taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla,” amesema Sanga.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali kutoka Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Aretas James Lyimo
ametumia nafasi hiyo kuieleza jamii kuwa michezo ni sehemu salama inayosaidia vijana kuachana na matumizi ya dawa hizo.

Amesema bonanza hilo limekuja katika kipindi muafaka cha maadhimisho ya wiki ya kupambana na dawa za kulevya huku akieleza kuwa tatizo la dawa hizo ni tishio kwa uchumi na mustakabali wa vijana.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Msekela, amesema benki hiyo inajivunia kuwa mdau wa kudumu wa bonanza hilo, akieleza kuwa wamekuwa wakishirikiana na wabunge katika kuendeleza miradi kwenye majimbo yao, ikiwemo sekta ya elimu.

Alitolea mfano wa shule kubwa iliyojengwa na CRDB katika Wilaya ya Ilala, jambo lililopokelewa kwa pongezi na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu.