Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeanza rasmi vikao vyake leo jijini Dodoma, likifungua ukurasa mpya wa safari ya miaka mitano ya kusimamia sera, sheria na mipango ya maendeleo ya Taifa.
Katika kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya, wabunge wanatarajiwa kuchagua viongozi wakuu wa chombo hicho Spika na Naibu Spika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo,aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu, ndiye mgombea anayepigiwa upatu zaidi kuchukua nafasi ya Spika.
Aidha, nafasi ya Naibu Spika inatajwa kuenda kwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, ambaye ameibuka kuwa miongoni mwa majina yenye mvuto mkubwa kwa wabunge.
Baada ya uchaguzi wa viongozi hao, Bunge litapiga hatua nyingine muhimu ya kuidhinisha jina la Waziri Mkuu, hatua itakayofuatwa na uzinduzi rasmi wa Bunge jipya na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku chache zijazo.
Bunge hili jipya linatarajiwa kuwa na wajibu mkubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa dira ya maendeleo, utawala bora na usimamizi wa rasilimali za umma kwa maslahi ya Watanzania wote.


