Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha kiasi cha kiasi cha Sh 3,645, 912, 947,000,00 ( Trilioni 3.645) kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 kwa ajili ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Idhinisho hilo limefanyika leo Mei 20 bungeni jijini Dodoma muda mfupi baada ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax kufanya wasilisho la makadirio ya bajeti ya wizara hiyo ambapo alibainisha kuwa kati ya Fedha hizo Sh 3, 327,115,385, 000,00 ni kwaajili ya matumizi ya kawaida na Sh 318, 797,562,000,00 ni kwaajili ya matumizi ya maendeleo.

Dk Stergomena alieleza kuwa wizara inatarajia kufanya shughuli mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwemo kuimarisha jeshi kwa zana na  vifaa vya kisasa  na rasilimali watu, pia kuimarisha miundombinu katika kambi,vikosi na shule za jeshi.

Aidha ameeleza kuwa wizara imedhamiria kuimarisha mashirika na taaisisi za utafiti wa masuala ya kijeshi,kuimarisha viwanda katika sekta ya ulinzi na kuanzisha viwanda vipya kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Katika hatua nyingine waziri ameeleza kuwa wanakusudia kukuza ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) Jumuiya za kikanda na nchi mbalimbali na hivyo kuimarisha Diplomasia ya Ulinzi na maeneo mengine ya Kimkakati.

Baada ya Bunge kuipitisha bajeti ya wizara hiyo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema jeshi hilo litaendelea na utekelezaji wa  majukumu yake ya msingi ikiwa ni pamoja na kuhakisha usalama wa nchi unakuwa katika kiwango cha juu.