Sehemu kubwa ya Burundi haina umeme tangu Jumatatu, huku mji mkuu wa Bujumbura ukiwa umeathirika pakubwa wakati nchi hiyo pia ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta.

Wakazi wa baadhi ya vitongoji wamesema wanateseka kwa kuishi karibu wiki nzima bila umeme, maji au intaneti. Hayo yameripotiwa na shirika la habari la AFP likinukuu vyanzo kadhaa.

Benki zimetangaza kutokuwa na uwezo wa kutoa huduma huku wasimamizi katika Hospitali ya Prince Regent Charles wakizitaka familia kuchukua miili ya jamaa zao kutokana na ukosefu wa umeme katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Shirika la maji na umeme linalomilikiwa na serikali REGIDESO , limesema tatizo hilo linashuhudiwa kutokana na “kazi ya kuunganisha mitambo” ambayo inatarajiwa kuendelea hadi Agosti 14. Burundi ni taifa dogo la Maziwa Makuu na kulingana na Benki ya Dunia ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.