Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Mwanza

Wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan amezindua daraja la kihistoria katika nchi yetu. Daraja hili ni la Kigongo – Busisi, Mwanza, ambalo limepewa jina na John Pombe Magufuli. Daraja hili limejengwa kwa zaidi ya Sh bilioni 700. Kiasi hiki chote ni fedha za ndani.

Sitanii, kwanza naomba nimwombee rehema hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli. Mbali na hadithi yake ya kupanda pikipiki na mtumbwi aliokuwa aupande ukatumbukia ziwani, mimi ninalo moja kuu la kusema kuhusu Magufuli. Uwezo wa kufanya uamuzi.

Halikuwa jambo jepesi kufanya uamuzi wa kujenga daraja hili lenye urefu wa kilomita tatu. Daraja hili ambalo ni refu kuliko yote katika Afrika Mashariki, ni wazi ile kuwaza tu kulijenga, kulihitaji ujasiri. Mungu alimchukua likiwa limejengwa kwa asilimia 25.

Sitanii, baada ya kifo cha Dk. Magufuli ilikuwapo hatari kubwa ya miradi hii mikubwa kukwama. Hapa ndipo Rais Samia Suluhu Hassan alipotuonyesha ujasiri wa hali ya juu. Angeweza kusema hili lisubiri kwa muda, maana haikuwa sehemu ya mpango wangu. Na nikuhakikishie msomaji, sote tungekubali hoja hiyo.

Rais Samia angeweza kusema hajui hata fedha Dk. Magufuli alikuwa anazitoa wapi, maana kwa uhalisia wakati huo makusanyo yalikuwa madogo kuliko matumizi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa inakusanya Sh trilioni 1.5. Leo TRA chini ya Rais Samia inakusanya Sh trilioni tatu.

Mimi sitaki kuzungumzia urefu, uzuri na uimara wa daraja, bali dhana halisi ya kujitegemea. Moja tu niligusie. Daraja hili linapunguza muda wa safari kati ya Busisi na Kigongo kutoka wastani wa saa moja kama hakuna foleni ya magari hadi dakika 4.

Sitanii, kuna nyakati pale Kigongo – Busisi magari yalikuwa yanakaa hadi saa 8 kivuko kikiharibika. Njia hii ni fupi kutoka Bukoba kwenda Mwanza ukilinganisha na ile ya kupita Kahama – Isaka – Tinde – Shinyanga hadi Mwanza. Inapunguza zaidi ya kilomita 200.

Kukamilika kwa daraja hili kuwe mwanzo wa kujenga utamaduni wa nchi yetu kuwaza mambo makubwa. Nchi yetu sasa ianze kuwaza sera ya kupunguza ajali na foleni. Iwe sera ya taifa letu kuwa kila penye makutano ya barabara, liwepo daraja magari yapite chini na juu.

Tuanze kuwaza ujenzi wa njia nne kwa barabara kuu zote. Tunduma hadi Dar es Salaam, Dar es Salaam hadi Mwanza, Bukoba hadi Arusha, Dar es Salaam hadi Kilimanjaro; kote huko ziwe barabara nne – nne hadi sita. Najua msomaji utaguna kuwa gharama ni kubwa.

Ni kweli gharama ni kubwa ila tukiishawaza tukafanya uamuzi, basi na iwe sera yetu miaka yote kuanzia sasa kuwa kila tukijenga barabara tunajenga njia nne hadi sita. Tutaokoa maisha ya watu wengi yanayopotea ajalini. Kuanzia sasa tuguse kila linalowezekana. Hata daraja la Dar es Salaam – Zanzibar kilomita zipatazo 35 tuanze kuliwaza kwa uhalisia.

Nimeisoma Ilani ya CCM ya 2025 hadi 2030. Ilani hii inalenga kuanzisha ujenzi wa reli ya umeme kwa kuunganisha nchi nzima. Tusiogope. Tuianze miradi hii mikubwa. Jemedali Rais Samia amekwisha kuthibitisha kuwa inawezekana.

Tujiapize Watanzania kuwa hata kwa utaratibu wa ‘Build Operate and Transfer – BOT)’ tuuze hatifungani za Serikali. Fedha zimo mifukoni mwa wananchi. Tukiuza hatifungani za trilioni 20 kwa Watanzania, tutapata fedha nyingi, tutajenga barabara kila kona ya nchi hii, usafirishaji utarahisika na makusanyo ya mapato yataongezeka.

Leo Bandari ya Dar es Salaam ikisafirisha tani milioni 90, iwapo miundombinu itaimarishwa, kitakuwa chanzo kikubwa cha mapato. Itaweza kukusanya Sh trilioni 3 hadi tano kwa mwezi, hivyo tutapata Sh trilioni kati ya 40 na 50 kwa mwaka.

Rais Samia kwa kujenga daraja hili la Busisi kwa zaidi ya Sh bilioni 700, kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere la kuzalisha umeme megawati 2,115, kuendelea na ujenzi wa reli ya mwendokasi inayogharimu zaidi ya Sh trilioni 10, amethibitisha kuwa kumbe Watanzania tunaweza bila misaada ya wafadhili.

Ilani ya CCM ya 2025 – 2030 inahamasisha ujenzi wa kongani za viwanda, hapo ndipo pa nchi yetu kutokea. Tupambane tujenge viwanda vikubwa. Kwa kufanya hivyo kodi zitaongezeka, nchi yetu itakuwa tajiri. Tumwombe Mungu ampe maisha marefu Rais Samia, utendaji huu uliotukuka uzidi kunufaisha Watanzania.

Hongera Rais Samia kwa ujenzi wa daraja la Busisi, sasa tuelekeze nguvu kwenye reli na barabara za vijijini, maana Bwawa la Mwalimu Nyerere nalo tayari. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827