Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Hospitali ya CCBRT imeendelea kutoa huduma ya macho na ushauri nasaha kwa wakazi wa Dar es Salaam katika Kituo cha Afya cha Anglikana kilichopo Buguruni, Manispaa ya Ilala kwa siku mbili mfululizo ikiwa ni sehemu ya kuwapa furaha wale wote wenye matatizo ya macho.
Akizungumza kwa nyakati tofauti pembezoni mwa zoezi la upimaji macho, Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Jamii na Utafiti, Bi. Rhoda Ndakwe amesema zoezi hilo ni endelevu na kwamba linafanyika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma.
“CCBRT imejiwekea utaratibu wake kutoa huduma ya macho na ushauri ili kusaidia jamii kukabiliana na matatizo ya macho,” Alisema Bi. Rhoda kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Bi. Brenda Msangi.

Amesema zoezi hilo la upimaji macho na utoaji ushauri nasaa bure limefanywa na hospitali hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Christian Blind Mission (CBM) limepata mafanikio makubwa kutokana na watu wengi kujitokeza kupima macho.
“Huduma hii inatolewa bure na itaendelea katika Wilaya nyingine zote za mkoa wa Dar es Salaam zikiwemo Temeke, Kigamboni, Kinondoni na Ubungo pia,” Alisema Bi. Rhoda.
Akielezea zaidi kuhusu zoezi hilo Bi. Rhoda amesema CCBRT imekuwa ikitoa huduma hizo bure sehemu mbalimbali hapa nchini kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali wakiwemo CBM, Light For The World (LFTW).

“CCBRT kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inalenga kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya rika tofauti katika jamii yetu, kuhakikisha kila mtu anapata huduma muhimu za macho. Ndiyo maana tukaweka kambi ya siku mbili ili wakazi wa Ilala wapate huduma hii,” Alisema Bi. Rhoda.
Hospitali ya CCBRT ni miongoni mwa hospitali chachen hapa nchini zinazotoa pia huduma mbalimbali za kibobezi zikiwemo Huduma za macho, huduma za figo na usafishaji Figo, huduma za mifupa, Huduma za uzazi na magonjwa ya wanawake, huduma za upasuaji pamoja radiolojia na nyingine nyingi.




