CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Frelimo cha Msumbiji vimekubaliana kuwashirikisha vijana ili wafahamu uhusiano uliopo kati ya vyama hivyo na kuhakikisha wananchi wa mataifa hayo wanakuwa na uhuru wa kiuchumi.
Pia, vimekubaliana kutengeneza fursa za ajira, hasa kwa kundi la vijana ambalo baada ya kupata elimu kupitia shule na vyuo walivyojenga wanahitaji kuwezeshwa ili wawe na njia zao za kujitegemea.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Machi 6, 2026, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Frelimo, Shakil Aboobacar, katika makao madogo ya chama hicho Lumumba, amesema wamekubaliana kushirikisha vijana kwa kuwa asilimia 65 ya wananchi wa mataifa hayo mawili ni vijana ambao hawaufahamu vizuri uhusiano na mapambano yaliyokuwepo.
“CCM na Frelimo lazima tuwe pamoja katika kutetea maslahi ya nchi zetu na kuhakikisha vijana wanapewa nafasi kubwa katika maendeleo ya mataifa yao. Hilo ndilo jambo kubwa tulilokubaliana,” amesema.

Wasira amesema Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameunda wizara maalum ya kushughulikia changamoto za vijana na kulinda maslahi yao.
“Tumeafikiana kuwashirikisha vijana si tu kwa kuwapa elimu ya kuwaajiriwa, bali pia elimu itakayowawezesha kujitegemea na kujiajiri wenyewe kwa kutumia sayansi na teknolojia,” amesema Wasira.
Amesema vijana wanapaswa kufahamu kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji ulijengwa kwa gharama kubwa.
“Tulilipa gharama ya damu. Uhusiano wetu na Msumbiji ni wa damu. Kama kuna uhusiano unaoweza kuandikwa kwa dhahabu, basi huu wetu unaandikwa kwa damu kwa sababu tulishirikiana katika mazingira magumu,” amesema.
Amesema baada ya kufikia hatua hiyo ni vigumu kusahauliana, huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa kizazi cha sasa kuendeleza uhusiano huo, hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 65 ya wananchi wa Tanzania na Msumbiji ni vijana.
“Hatuwezi kuwaelewesha vijana sababu za mapambano yaliyofanyika, watu waliokufa na jitihada zilizofanyika wakati wa kutafuta uhuru, kama hatutawashirikisha. Wajibu wetu kama vyama ni kuwashirikisha vijana. ” amesema.
Kwa upande wake, Aboobacar amesema wamekutana ili kuimarisha ushirikiano na kupata nguvu mpya katika kukabiliana na changamoto za sasa, hasa kuhakikisha vijana wanapata maisha bora.
“Haitawezekana kuajiri vijana wote, lakini tuna wajibu wa kuweka mazingira mazuri yatakayowawezesha kujiajiri. Ni muhimu kuwapa elimu yenye ujuzi na kutengeneza mazingira rafiki ili vijana wetu waweze kuibua uwezo wao na kujitegemea,” amesema.

Amesema ni muhimu kwa vyama hivyo kushirikiana kama ilivyokuwa wakati wa mapambano ya kupata uhuru ili kukabiliana na changamoto mpya za kiuchumi, ikiwemo kuunda fursa zaidi za ajira kwa vijana.
“Mapambano ya kupata uhuru yalituwezesha kufikia hatua tuliyopo leo. Sasa tuna vijana wengi waliopata elimu kupitia shule na vyuo tulivyovijenga, hivyo tunapaswa kuwawezesha ili waweze kujitegemea kiuchumi,” amesema.
Amesema kuwa, ingawa haiwezekani kuajiri vijana wote, ni wajibu wa serikali na vyama kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha kujiajiri kwa kutumia elimu na ujuzi walioupata.
WASIRA NA HISTORIA YA USHIRIKIANO
Katika hatua nyingine, Wasira amesema Chama cha Frelimo ni mshirika wa karibu wa CCM, akieleza kuwa kilizaliwa Tanzania na mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kukianzisha alikuwa Edward Mondlane, ambaye aliishi Dar es Salaam, ingawa alifariki kabla ya Msumbiji kupata uhuru.
Amesema Tanzania ilipata uhuru mapema kabla ya Msumbiji, na wakati huo Mwalimu Julius Nyerere alikuwa anaamini kuwa uhuru wa Tanzania hauwezi kukamilika ikiwa kusini mwa nchi hiyo bado kunatawaliwa na Wareno.
“Ni kweli kuwa wakati Wareno wanatawala Msumbiji walikuwa wanaungwa mkono na Makaburu wa Afrika Kusini. Walipoona Tanzania ni adui yao, walianza kufanya mashambulizi katika maeneo ya Msumbiji na Mtwara,” amesema.
Ameongeza kuwa baada ya Mondlane kufariki kabla ya kupatikana kwa uhuru wa Msumbiji, Samora Machel alichukua jukumu la kuendeleza mapambano.

“Baada ya Msumbiji kupata uhuru, Samora aliaga Dar es Salaam akielekea kuwa Rais wa Msumbiji. Mapambano yalikuwa makali, lakini CCM na Frelimo walishirikiana kwa karibu kuhakikisha Msumbiji inapata uhuru,” amesema.
Wasira amesema wakati CCM inaanzishwa mwaka 1977 alikuwa na umri wa miaka 31, na kwamba mkutano wao na viongozi wa Frelimo unalenga kuhakikisha vyama hivyo vinaendelea kuwa vya vijana kwa kuendeleza misingi iliyoasisiwa na waasisi wao.
“Wakumbuke kuwa Mondlane aliuawa akiwa anapigania haki na alikuwa kijana. Vijana wa sasa watakuwa wamekosea kama watasahau historia hiyo. Lazima wajue kuwa Mondlane aliuawa akiwa nje ya nchi yake,” amesema.
Ameongeza kuwa hata Samora Machel alifariki katika ajali ya ndege, akidai kuwa waliokuwa wanapinga mapinduzi ya Msumbiji ndio hao hao waliokuwa wanapinga mapinduzi ya Tanzania kupitia CCM.



