Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kimeanza mpango wa kurahisisha upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ili kupunguza kero kwa wananchi, hasa wa maeneo ya pembezoni.

Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Mwalimu Mwajuma Nyamka, alisema hayo wakati alipoanza ziara yake ya kushukuru wananchi wa Kata ya Mbwawa kwa kukiunga mkono chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita.

Akiwa ameambatana na Wataalamu wa RITA alieleza awali wananchi wengi walilazimika kufuata huduma za vyeti vya kuzaliwa mjini Kibaha, hali iliyokuwa ikiwapa usumbufu mkubwa.

“Ni jukumu letu kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi,tunawashukuru RITA kwa kukubali kushuka hadi ngazi ya jamii,” alisisitiza Nyamka.

Aidha, aliwataka wanachama na viongozi wa CCM kudumisha umoja baada ya uchaguzi, akisisitiza kuwa mshikamano ni msingi wa kukiimarisha chama.

Vilevile Nyamka alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM kupitia miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu na umeme.

Alihimiza viongozi wa chama kuendelea kuingiza wanachama wapya na kuwafikia wananchi moja kwa moja badala ya kusubiri kipindi cha uchaguzi.

Kwa upande wake, mkazi wa Mbwawa, Saidi Ngamba, alishukuru kusogezwa karibu kwa huduma za RITA na kuomba zoezi hilo lisimamiwe kwa ufanisi ili kusiwe na ubabaishaji.

Naye Msajili Mwandamizi wa RITA Wilaya ya Kibaha, George Chuwo, alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo, akieleza kuwa waombaji wanapaswa kuwa na nyaraka muhimu, ikiwemo vitambulisho , barua za utambulisho na ada ya usajili wa cheti cha kuzaliwa ni Shilingi 20,000.

Katika ziara hiyo, Nyamka aliwatembelea baadhi ya mabalozi wa mashina, akiwemo Salehe Ramadhan wa tawi la Miswe Chini, aliyejeruhiwa na mamba hivi karibuni, ambapo anaendelea na ziara hiyo katika kata 14 za wilaya huku april 10 akitazamiwa kufanya ziara kata ya Visiga.