*Balozi Nchimbi atoa neno, akimwakilisha Dkt. Samia msibani

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kitabu alichoandika Alhaj Mzee Mohamed Mustafa Songambele kitakuwa mojawapo ya rejea adhimu za historia ya Tanzania.

Balozi Nchimbi amesema kuwa kitabu hicho kiitwacho “Safari ya Karne”, kina utajiri wa maelezo kuhusu mapambano ya kutafuta uhuru wa Tanganyika, kupatikana kwa nchi na taifa la Tanzania na kuundwa kwa CCM.

Dkt. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akitoa salaam za pole na rambirambi kwenye msiba wa Hayati Alhaji Mzee Songambele, akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mjini Songea, mkoani Ruvuma, leo Jumatatu tarehe 2 Juni 2025.

“Kutokana na heshima na mchango mkubwa wa Mzee Songambele kwa nchi yetu, taifa letu na chama chetu, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuguswa sana na msiba huu, ameniagiza rasmi kumwakilisha na ameagiza Chama na Serikali kuchukua gharama zote za msiba huu.

“Mzee Songambele amefariki akiwa amemaliza kuandika kitabu chake. Hadi mwezi Machi mwaka huu, alikuwa amekiita jina la “Swahiba wa Nyerere”, lakini miezi miwili iliyopita akabadili, nadhani aliona atatimiza miaka 100, akakiita “Safari ya Karne,” amesema Balozi Nchimbi na kuongeza;

“Kutokana na umuhimu wa kitabu hicho, ambacho aliniomba niandike dibaji na niliandika, humo ameelezea mengi kuhusu yeye na Nyerere, harakati za uhuru, utaifa wetu na CCM pia, Chama Cha Mapinduzi kitasimamia ili kitabu hicho kitoke ili Watanzania wapate kujifunza historia vizuri,” alisema Balozi Nchimbi.

Aidha, Balozi Nchimbi alisema Mzee Songambele pia alikuwa mmoja wa viongozi waliotoa mchango mkubwa kwa nchi, taifa, chama na serikali kutokea Mkoa wa Ruvuma, akisisitiza kuwa hilo ni jambo linalostahili kuenziwa na viongozi wa kizazi cha sasa kwa kuwa waadilifu, wanaowajibika, wazalendo kwa nchi na kuwatumikia watu.

Hayati Alhaji Mzee Songambele, mwanasiasa na kiongozi mkongwe nchini, ambaye alifariki usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 1 Juni, mwaka huu, alizikwa Jumatatu Juni 2, 2025 katika makaburi ya familia yaliyoko Bombambili, mjini Songea.