Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani kimesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha kuthamini mchango wa wazee katika Taifa kupitia ushirikishwaji wao kama nguzo muhimu ya hekima.

Pia kimedai kuwa Rais ameendelea kuonesha uzalendo wa kweli katika kulipigania nchi.

Akitoa tamko kwa waandishi wa habari mjini Kibaha, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Pwani, David Mramba, alisema chama hicho kinaunga mkono maelekezo, maono na msimamo wa Mheshimiwa Rais kama alivyoeleza katika hotuba yake ya Disemba 2, 2025 alipozungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam hotuba ambayo, kwa mujibu wa CCM, imeiweka nchi katika mwelekeo sahihi wa maendeleo.

Mramba alisisitiza umuhimu wa kulinda amani, akitaja kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa.

Aidha, alisema hotuba hiyo imeeleza maono ya kimkakati ya kuendeleza mageuzi ya kiuchumi na kijamii, kwa kuimarisha sekta mbalimbali pamoja na huduma za kijamii.

Hata hivyo, alifafanua kuwa CCM inaunga mkono hotuba hiyo kwa sababu imeweka mwelekeo sahihi kwa Taifa, ikisisitiza mshikamano na kuongeza fursa za ajira kwa makundi maalum, vijana na wanawake.