Na Allan Kitwe, Tabora
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora kimeridhishwa na maboresho makubwa ya miundombinu ya afya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya zote za Mkoa huo hali iliyopelekea wananchi kuanza kupata huduma bora.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Saidi Juma Nkumba alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili baada ya kuhitimishwa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa katika wilaya zote.
Amesema kuwa huko nyuma vituo vingi vya kutolea huduma za afya katika Mkoa huo vilikabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwemo uchakavu wa miundombinu, ukosefu wa dawa na vifaa tiba vya kutosha na uchache wa watoa huduma.
‘Katika kipindi cha miaka 5 ya serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan miundombinu ya afya imeboreshwa kwa kiwango kikubwa sana ikiwemo kujengwa hospitali mpya kila wilaya na vituo vya afya’, amesema.
Nkumba amebainisha kuwa Chama Cha Mapinduzi kina kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta hii na sekta nyinginezo kwa kuwa yamesaidia kupunguza malalamiko ya wananchi na sasa wanafurahia huduma.
Ametoa mfano wa Kituo cha afya Ulyankulu cha Wilayani Kaliua ambacho kilijengwa miaka ya 1970 na miundombinu yake ilikuwa kimechakaa sana lakini serikali ya awamu ya 6 imekifanyia maboresho makubwa na sasa kinapendeza.
Aidha kujengwa kwa hospitali mpya za wilaya na kuboreshwa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Kitete, kumeleta neema kubwa kwa wananchi kupata huduma zote wanazohitaji hivyo kuwapunguzia adha ya kwenda hospitali kubwa za Bugando na Muhimbili.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa, Wilson Nkambaku amepongeza serikali ya CCM ya awamu ya 6 kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa asilimia 100 katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji na nishati.
Ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi na serikali yake na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu wawachague wagombea wa CCM.


