Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kufanya harambee kwa ajili ya kutafuta shilingi Bilioni 100 za kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Chama hicho Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema harambe hiyo itafanyika kuanzia saa 11 jioni kesho Agosti 12, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Dkt. Nchimbi alisema kuwa hadi sasa chama kimesajili kadigitali wanachama zaidi ya milioni 13, hivyo aliwahimiza wanachama hao na wapenzi wa Chama hicho kutumia saa 28 hadi kufikia kesho kuonesha nguvu yao katika kuhakikisha wanakichangia Chama chao ili kiweze kufanya kampeni zake vizuri.

“Kama mnavyojua mwaka huu Oktoba tutapiga kura baada ya kampeni ili kupata Rais, Wabunge na Madiwani. CCM pia kinashiriki kikamilifu katika nafasi hii, kwa kila Chama kinapoenda kwenye uchaguzi kina kuwa na maandalizi ya Kampeni,” alisema Dkt. Nchimbi na kuongeza,

“Kampeni zinahitaji fedha kwa ajili ya Mafuta ya Magari, Mabango, Tisheti na Kanga na malengo ni kutafuta shilingi Bilioni 100, na Wana CCM wajue tunalenga kiasi hicho. Hivyo kesho (leo) ndiyo siku ya wanachama kuonesha nguvu yao,”.

Kwamba mgeni Rasmi katika harambee hiyo atakuwa ni Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo alieleza utaratibu wa wanachama na wapenzi wa Chama hicho kuweza kutuma michango yao kuwa ni kupitia  jina la Account ambalo ni KATIBU MKUU WA CCM UCHAGUZI HARAMBEE ambapo aliitaja Accont Namba: 0150001GMMT00 CRDB Benki.

Kwamba kwa mitandao yote ya Simu ni kwa kutumia Mosi, *150*50*1# na kisha kuingiza Control Namba: C02025 na mwisho kuweka kiasi cha fedha ambacho mwanachama ama mpenzi wa chama hicho atahitaji kuchangia.

Dkt. Nchimbi alitaja njia ya pili ni Lipa kupitia CRDB Sim Banking, NMB Mobile, Selcom Pay na NBC Kiganjani, Kwamba mchangiaji atakwenda kwenye Payment na kuchagua CCM na kisha kuingiza Control Namba: C02025.

Aidha Dkt. Nchimbi alieleza kuwa watafurahi hata vyama vingine vya siasa kama vitawachangia.