Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, kimetangaza rasmi majina ya wagombea watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa nafasi za Ubunge wa Majimbo, Viti Maalum na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

CPA Makalla amesema uteuzi huo, uliofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, umehusisha majimbo 272 upande wa Tanzania Bara na umehitaji umakini mkubwa kutokana na wingi wa maombi ya wagombea.

“Majimbo zaidi ya elfu tano yalipokea maombi ya wagombea,Kazi hii ilikuwa kubwa na ilihitaji umakini mkubwa ,Kwa wale ambao hawajapata uteuzi, tunawaomba waendelee kuwa watiifu kwa chama kwani bado CCM inawathamini,” amesema CPA Makalla.

Katika orodha hiyo, baadhi ya vigogo akiwemo Luhaga Mpina, January Makamba ,Askofu Josephat Gwajima na Mrisho Gambo hawajarejea kwenye majina ya mwisho ya wagombea, hatua inayotafsiriwa kama mabadiliko makubwa ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, mchakato huo pia umefungua milango kwa sura mpya ambapo watu maarufu wakiwemo wasanii na wanahabari wamepata nafasi ya kugombea.

Wanahabari Salim Kikeke amepitishwa kugombea Jimbo la Moshi Vijijini, msanii Baba Levo na mwanahabari Baruan Mhuza wamepata nafasi ya kugombea katika Jimbo la Kigoma Mjini, hatua iliyopokelewa kwa hisia mpya za matumaini kwa vijana na wadau wa sekta za sanaa na habari.

Taarifa za awali zinaonyesha majimbo kama Arusha Mjini yalikuwa na wagombea 7, Dodoma Mjini wagombea 8, Mtumba wagombea 4, Busanda wagombea 4 na Chato Kaskazini wagombea 5.

CPA Makalla amesisitiza kuwa vigezo vya uadilifu, uwezo wa uongozi na kukubalika kwa wananchi vilizingatiwa ili kuhakikisha chama kinapata wagombea bora watakaotekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM na kuendeleza kasi ya maendeleo ya Taifa.

Wagombea waliopitishwa wanatarajiwa kuanza maandalizi ya kampeni rasmi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, huku CCM kikiahidi kampeni za kistaarabu zinazolenga masuala ya maendeleo kwa Watanzania wote.