Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemkabidhi hati ya umiliki wa nyumba Mjane wa Marehemu Justus Rugaibura, Alice Haule, baada ya Tume maalum ya Serikali kubaini kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo iliyokuwa katika mgogoro wa muda mrefu na mfanyabiashara Mohamed Yusufali.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Oktoba 20, 2025 jijini Dar es Salaam, kufuatia kukamilika kwa uchunguzi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu umiliki wa kiwanja namba 189 kilichopo Msasani Beach, Kinondoni.

Akiwasilisha ripoti ya uchunguzi huo kwa Mkuu wa Mkoa, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukurani Kyando, amesema timu ya wataalamu wa ardhi ilipitia nyaraka zote, kuwahoji wahusika na kuchambua mwenendo wa mauziano kati ya pande husika.
“Kamati imebaini kuwa mikataba ya mkopo na mauziano kati ya marehemu Rugaibura na Yusufali haikuwahi kuwasilishwa rasmi wizarani kama taratibu zinavyotaka, jambo lililosababisha utata wa kisheria katika umiliki wa kiwanja hicho,” amesema Kyando.
Ameongeza kuwa wakili aliyeshiriki katika mchakato huo alikiri kuwa marehemu Rugaibura ndiye aliyekuwa anaratibu saini ya mkewe, lakini nyaraka hizo hazikuwahi kurejeshwa kwa uthibitisho wa kisheria.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kamati ilihitimisha kuwa umiliki huo ulikuwa na dosari kubwa na ikapendekeza mamlaka husika zichukue hatua kwa mujibu wa Sheria za Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999.
Baada ya kupokea ripoti hiyo, RC Chalamila alimkabidhi Alice hati ya nyumba pamoja na Shilingi Milioni 10 kutoka serikalini kama mtaji wa kuanzisha shughuli zake za kiuchumi baada ya kipindi kigumu cha mgogoro huo.
“Serikali haitakubali kuona mwananchi anatapeliwa au kunyanyaswa kutokana na udhaifu wa mifumo. Kesi ya Bi. Alice ni mfano wa namna Serikali ilivyo makini katika kulinda haki za wananchi wote bila upendeleo,” amesema Chalamila.

Chalamila ameongeza kuwa hatua hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kusimamia haki na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Alice ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo, ambapo amesema: “Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa kimbilio la wanyonge. Leo napumua kwa amani baada ya miaka ya mateso na hofu. Naomba wananchi wengine waamini Serikali yao, wasikate tamaa.”

