Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimewataka wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu na kufichua kuwa kususia uchaguzi ni kukwamisha maendeleo.

Rai hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho Salum Mwalimu alipokuwa akihutubia wakazi wa Tabora katika uwanja wa shule ya sekondari Uyui mjini Tabora.

Alisisitiza kuwa wananchi wana haki ya kushiriki uchaguzi huo bila kuogopa wala kutishwa na mtu yeyote ili kutimiza haki yao ya kikatiba, akabainisha kuwa kususia uchaguzi ni kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

‘Kutofautiana mitazamo ndio demokrasia yenyewe na ni jambo la kawaida, hatupaswi kununiana wala kutiana hofu, wananchi wanataka mabadiliko ya kweli siyo ubabaishaji wala malumbano,’ alisema.

Mwalimu alisema kuwa CHAUMMA ni chama cha ukombozi wa wananchi, na suala la kutafuta ukombozi ni safari ndefu yenye mapito mengi, taifa linahitaji mabadiliko ya kweli ili wananchi wapate haki yao.

Alibainisha kuwa dosari zote zilizoripotiwa katika taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hivi karibuni zinapaswa kufanyiwa kazi nna wote walioisababishia hasara serikali wote wachukuliwe hatua.

Yote yaliyobainishwa katika taarifa hiyo yanaonesha utendaji mbovu wa baadhi ya Maafisa na Watumishi wa Serikali, ukosefu wa maadili, Viongozi bora, imara na wenye uzalendo kwa rasilimali za nchi yetu,’ alisema.

‘Hayati Maalimu Seifu ni gwiji wa siasa za mageuzi na ni shujaa wa kuigwa, naomba tuige ushujaa wake, tuikosoea serikali pasipo kuogopa mtu ili kuhakikisha inawatendea haki wananchi na kutoa fursa kwa wote’, alisema.

Awali Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Devota Minja alisema kuwa wananchi wakikipa ridhaa chama hicho kushika dola, watahakikisha kodi kandamizi zote zinafutwa ili kuendana na sera yao ya ‘ubwabwa’kwa wote.

Alisema kuwa sera yao inasisitiza lishe kwa watu wote na ni mkakati wa kuondokana na utapia mlo kwa kuisambalatisha kwa wananchi ambapo watapambania kilimo madhubuti cha mpunga ili chakula kipatikane kwa wote.

‘Naomba muipe CHAUMMA nafasi ya kushika dola ili kiwapambanie na kuwa na uhakika wa maisha na maendeleo endelevu yanayoonekana ambapo kila mwananchi atafurahia kwa kunufaika na siyo maneno ya faraja tu.

Alisisitiza kuwa CHAUMMA imedhamiria kupigania ukombozi wa wananchi na kuhakikisha wanakuwa na uhuru na amani ya kweli ikiwemo kupata huduma zote za kijamii ambazo ni haki yao ya msingi.