Na Jovina Massano, JamhuriMedia, Musoma
VIONGOZI wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) wamewaahidi kuwapambania wananchi katika kudai mabadiliko mbalimbali ya Sheria.
Wamewaeleza hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mukendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara .
Mkutano huo ni muendelezo wa mikutano ya chama hicho kuwafikia wanachama na wananchi huku wakinadi sera zenye maslahi ya wananchi.

Aidha wameahidi kupigania dhamira ya wananchi ili kuleta mabadiliko kwa kutosusia uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu..
Katibu mkuu wa CHAUMA Taifa Salum Mwalim amewaelezea wananchi madhara ya kutoshiriki uchaguzi mkuu kwa vyama cya siasa hapa nchini
“Kutoshiriki uchaguzi mkuu kunaondoa uhalali kwa wananchi kwa kukimbia Jukwaa la ushindi na kuwarudisha mahala wasipopahitaji na kutoa ushindi kwa urahisi usipoingia kwenye uchaguzi unakosa nguvu ya kukiendeleza chama”,amesema Salum.
Ametoa mfano wa madhara ambayo yaliathiri Chama Cha Wananchi (CUF) pale kilivyojiondoa kwenye uchaguzi na kurahisisha Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi mkubwa na kupata viti vingi vya uongozi.

Amesema chama cha siasa akijengwi na kauli kali kali bali huundwa sera na mikakati yenye kujibu haja za wananchi kulingana na mahitaji husika.
Nae Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara Devota Minja amesema ili kuondoa Sheria mbovu ni lazima ushiriki uchaguzi na kuandaa hoja thabiti zenye kuleta mabadiliko kwa wote.
“CHAUMA wamedhamilia kuwafikia wananchi wote ili wapate ukombozi thabiti wa kifikra”, amesema Devota
CHAUMA wameahidi wananchi na wanawama kuwa kuelekea uchaguzi mkuu wataweka wagombea wenye ushawishi mkubwa katika nafasi zote za Rais,ubunge na udiwani.

