Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeahidi kutunga sheria ya matumizi ya akili unde ndani ya siku 100.

Kupitia ilani yake yam waka 2025/2030 kimesema sheria hiyo itakuwa kwa ajili ya maendeleo ya watu wote na si kuwaadhibu watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Ilani hiyo imesema sharia hiyo itahusu matumizi ya akili unde katika shule na vyuo bila kuathiri masuala ya ubunifu na uwezo wa wanafunzi kufikiri upya ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayokuwa kwa kasi duniani.

Pia imesema itaundwa tume ili kuondoa tatizo la mauaji ya wananchi wanaoishi au kupakana na mamlaka za wanyamapori au mamlaka za misitu na mamlaka nyingine zinazohusika na masuala hayo.

Aidha, kimeeleza tume hiyo itachunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa muda mrefu imelitafuna taifa katika maeneo mbalimbali bila kuwa na ufumbuzi wa kudumu.

Pia Chaumma imeeleza katika siku 100, serikali yake itaanzisha na kuzindua mkakati wa mfumo bora wa lishe kuanzia kwa watoto wadogo katika ngazi ya elimu ya awali, wanafunzi shuleni na wagonjwa katika hospitali za umma. Mkakati huu utaitwa Ubwabwa kwa wote.